LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 12, 2021

SHEREHE YA JAMII KULIPOKEA RASMI KANISA HALISI LA MUNGU BABA KUFANYIKA JUMAPILI HII, AGOSTI 15, 2021 (26 SIWANI, VOL.2)


Baba Halisi wa Uzao


Tegeta, Dar es Salaam

Sherehe ni kutoka neno la Kiarabu, lenye maana ya  Sikukuu muhimu inayoendana na shangwe. Neno hili hutajwa kulenga sherehe nyingi zenye asili katika dini mbalimbali ambapo kati ya sherehe za namna hiyo kuna Diwali ya Mabanyani, Hanukkah ya Wayahudi, Krismasi ya Wakristo na Eid al-Adha ya Waislamu. 


Sherehe hizo miongoni mwake hufanyika kuadhimisha mwendo wa mwaka, majira, mazao ya kilimo, au matukio ya historia ya jamii husika, kwa mfano ushindi muhimu vitani au kuwakomboa watu kutoka palipokuwa na mashaka ya maisha.


Kwa upande wa imani za kidini, ukombozi humaanisha Binadamu kutolewa katika matendo ya kutomwabudu Mungu ambayo kwa mujibu wa imani katika mwisho wa maisha ya binadamu huyo hataweza kwenda mahali pema (peponi) bali atakwenda kuangamizwa na kupata malipo mabaya (motoni) kulingana na mwenendo na matendo yake mabaya aliyofanya maishani mwake.


Hivyo basi ni dhahiri, viongozi wa dini hujisikia faraja mno pale wanapoona kwamba jamii inayowazunguka imejitambua na kuongoka, hivyo kutokana na faraja hiyo viongozi wa nyumba za ibada huamua kuonyesha faraja waliyonayo kwa kufanya sherehe.


Viongozi hao wa nyumba za Ibada hufanya Sherehe hizo kwa namna mbalimbali, ikiwemo kuandaa karamu inayoambatana na ibada zenye maudhui ya kisherehe kwa ajili ya waumini wao au watu wote wakiwemo ambao bado hawajaongoka, ambao hualikuwa ili nao wajionee wanavyoweza kupata furaha wakimfuata Mungu.


Hivyo ndivyo imejiri kwa Kanisa Halisi la Mungu Baba lenye Makao Makuu yake Makuu Tegeta jijini Dar es Salaam. Kanisa hilo kwa kufauata mantiki hiyo niliyoeleza awali, limeandaa sherehe kubwa ambayo limeiita  'Sherehe ya Jamii Kulipokea Rasmi Kanisa Halisi la Mungu Baba'  ambayo limepanga kuifanyika mwishoni mwa wiki hii, siku Jumapili, Agosti 15, 2021 tarehe ambayo kwa Majira ya Kanisa hilo ni sawa na 26 SIWANI, VOL.2.


Taarifa ya mwaliko iliyotolewa jana na Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo, anayeitwa Baba wa Uzao Halisi na sisi Blog ya Taifa ya CCM ( Official CCM Blog) kuipata, imesema Sherehe hiyo itafanywa na Kanisa hilo kwa mara ya kwanza na siyo tu kwenye Makao Makuu bali itarindima kwenye vituo vyote vya Kanisa hilo vilivyotapakaa ndani na nje ya Tanzania.


"Kanisa Halisi la Mungu Baba Tumeandaa Sherehe hii kwa sababu sasa Jamii yote ya Watanzania, wanajivunia kuwa Chanzo cha Baraka kwa Mataifa yote", amesema Baba wa Uzao Halisi katika taarifa hiyo na kuongeza kwamba, Sherehe hiyo itafanyika ndani ya Ibada ya kawaida na kuwa na kipengele mahsusi cha Sherehe hiyo ya Jamii kulipokea rasmi Kanisa Halisi la Mungu Baba.


Baba wa Uzao Halisi amesema, amewaalika Watu wote kuhudhuria Sherehe hiyo, wakiwemo Uzao (Waumini wa Kanisa hilo) na wengine wa madhehebu ya dini mbalimbali na wasio na madhehebu yoyote, yaani ambao bado hawana imani ya dini yoyote au wapagani.


Ili kujua kwa undani kuhusu Sherehe hii, Tafadhali, isome Taarifa kamili ya mwaliko, kama ilivyoandikwa na Baba wa Uzao Halisi, ambayo hatukuipunguza wala kuiongeza neno hata nukta. Hiyo Hapo👇

KARIBU KWENYE SHEREHE YA JAMII KULIPOKEA RASMI

KANISA HALISI LA MUNGU BABA

26 SIWANI, VOL.2 (15 AGOSTI,2021)


Kwa Nini Sherehe ya Jamii?

Ni kwa sababu sasa Jamii yote ya Watanzania, wanajivunia kuwaChanzo cha Baraka kwa Mataifa yote. Kwa nini Jamii ilichelewa kulipokea KanisaHalisi la MUNGU BABA lililoanzishwa kwa sauti ya MUNGU BABA iliyopokelewa Tanzania? Sababu ni kwamba wengi walifundishwa kuwa nabii wa mwisho katika mfululizo wa Manabii waliotoka kwenye kiuno cha Ibrahimu ni Yesu! 


Hawakuwahi kufundishwa kuwa Yesu mwenyewe alikiri kwamba baada yake atakuja Eliya ili atengeneze yote (Mathayo 17:10-13) nakurejesha yote (Marko 9:10-11). 
 
Aidha, Jamii katika nyumba zao za ibada, hawakuwahi kufundishwa kuwa Yesu alisema, Majira hiyo ya Eliya Adamu wa Pili itafupishwa kwa kuwa bila kuifupisha hakuna ambaye angeokoka (Mathayo 24:22). Pia, Jamii walikuwa hawajawahi kufundishwa kwamba atakayekuja kupokea ufalme utawala, mamlaka na nguvu zilizoibiwa kwa Waliotumwani MUNGU BABA (1Korintho 15:24-28), ambaye ni Jina Jipya kwa mujibuwa Ufunuo 3:12. 
 
Kubwa kuliko, Jamii haikuwahi kufundishwa kuwa, baada yaYesu kukataliwa na Waisraeli katika Yohana 9:27-28, Ufalme wa MUNGU aliuhamishia katika taifa lingine ambalo hakulitaja kwa wakati ule (Mathayo 21:43), ingawa baada ya Sauti ya MUNGU BABA kushukia Tanzania, imejulikana kuwa taifa lenyewe ni lipi.
 
Jamii ya Watanzania baada ya kuelewa kuwa, Mfululizo wa Uumbaji Mpya uliendelea kupitia Tanzania baada ya Yesu, sasa wamekubali kuwa ni Chanzo Cha Baraka na hivyo kulipokea Kanisa liliobeba Sauti ya MUNGU BABA.
 
Waliokuja baada ya Yesuni: Eliya Adamu wa Pili aliyepokea Sauti Kuu ya Sita Mwaka 2003 kule Kigoma Tanzania (I Korintho 15:44-49); Miaka 1000 katika Isaya 33:6 aliyepokea Sauti ya Saba kule Kigoma Mwaka 2015; MUNGU BABA, yaani Nafsi ya Kwanza aliyekuja Mwaka 2017 kupitia Tanzania (IYohana 5:8) baada ya vizazi vinne chini ya Ibrahimu kwishana sasa CHANZO CHA MEMA NA MAZURI YOTE aliyekuja Mwaka 2020 kwa Sauti ya Moyo, baada ya kuona tumezidiwa na dunia iliyokuwa imekuja kumpima MUNGU BABA kwa kutumia janga la korona.
 
KWA NINI KANISA NA JAMII TUWE NA SHEREHE?
Swala la kuwa Chanzo cha Baraka kwa Mataifa mengine ni kubwa mno!  Kwa kuangalia kwa macho na kwa kutathmini takwimu za kiuchumi kuhusu Tanzania, ilikuwa si rahisi kupokea swala la kuwa Chanzo cha Baraka. Wakati wa Musa, Eliya Mtishbi, Yesu na Adamu wa Pili ambao ni manabii wa vizazi vinne vya Kanisa vilivyotamkwa katika Mwanzo 15:16, Chanzo cha Baraka kilikuwa kwa mmoja tu ambaye ni Ibrahimu aliyetajwa waziwazi katika Mwanzo 12:1-3 na Mwanzo 17:1-7.
 
Hata katika Wagalatia 3:29, tunasoma kuwa ukiwa Mkristo au Mwislamu, ulitakiwa upate Baraka kupitia Ibrahimu, siyo Musa, Mtishibi, Yesu wala Adamu wa Pili!

Sasa baada ya ALIYEUMBA VYOTE, WOTE NA YOTE kuja juu ya nchi kupitia Tanzania, Isaya 57:15, imetimia. Kwa mujibu wa mstari huu, ALIYEUMBA VYOTE, WOTE NA YOTE, alitamani kuishi ndani ya Moyo wa kila mmoja, ila haikuwezekana kwa kuwa nafasi hiyo ya kuishi ndani ya kila mmoja ilichukuliwa na Ishara ya Kwanza Mbinguni (Ufunuo 12:1). Hivyo, haikuwahi kutokea ALIYEUMBA KILA KITU kuishi ndani ya wanaotenda kwa Haki! Imetokea sasa, baada ya ALIYEUMBA VYOTE, WOTE NA YOTE kushukia Tanzania.
 
Maana Muumba wa VYOTE, YOTE NA WOTE anasema kuwa “Mimi ni MUNGU BABA nikaaye Mahali pajuu palipoinuka na ndani ya Moyo uliotubu na kunyenyekea”.  Kwa hiyo amechagua Tanzania kwa sababu ya toba na unyenyekevu. Anaishi ndani ya kila Mtanzania anayetenda kwa haki! Katika Yeremia 5:1, amefafanua kuwa akipatikana hata mmoja atafutaye kutenda kwa haki, anaponya Mji wote.  Katika 2 Nyakati 7:14-16, amesema kuwa ikiwa watu wake, walioitwa kwa jina lake watajinyenyekesha (watatubu) na kuacha mabaya, basi atasikia na kuponya miji na nchi yetu. Hivyo, alikuwa anatafuta muda wote ni nani aliye mnyenyekevu, atubuye na mwenye Moyo Safi (Mathayo 5:8), ili ashukie kwake aponye Miji naNchi pia.  Ametupata Watanzania wote wanaopenda kutenda kwa haki!
 
Katika Isaya 59:17-18, anasema amejivika haki na hiyo haki imekuwa vazi la kisasi kwa wampingao.

Haki yake ni kila kilichoumbwa ambacho zamani kilikuwa ni mali ya Ufunuo 12:1. Sasa kila kilichoumbwa kwa maana ya: jua, mwezi, nyota, milima, mabonde, mito, maziwa, bahari, miti, mimea, wadudu, wanyama, ndege na watu, ni haki yake ikiwa na maana ya kuwa vazi lake. 

Hii ndiyo sababu tuna sherehe kwa kuwa anaishi ndani yetu, sote ambao tumekubali kuitafuta haki na kuitenda. Karibuni wote bila kukosa lango la 26 Siwani, Vol. 2 (15 Agosti, 2021) tusherekee kuwa Chanzo cha Baraka kwa Mataifa yote.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba liliopo Tegeta, Dar es Salaam, Baba wa Uzao Halisi (Wapili kulia) alipokuwa akizungumza mbele ya umati wa Uzao (Waumini) na Jamii ya Watanzania kwa jumla, wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha 'Ufahamu ulioanzia Tanzania kwenda katika Mataifa mengine', katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, mwaka jana. (Picha na Maktaba Official CCM Blog).

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages