Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameshuhudia kuapishwa kwa Rais mpya wa Zambia Hakainde Hichilema katika sherehe mwanana ambayo imefanyika katika Uwanja wa Taifa wa Mashujaa (National Heroes Stadium) Jijini Lusaka Zambia leo.
Rais Samia ambaye kwenye sherehe hiyo alifuatana na Viongozi kadhaa akiwemo Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shakaka, alipata fursa ya kumsalimia na kumpongeza Rais Hichilema baada ya Rais huyo kuapishwa.
Viongozi wengine aliofuatana nao Rais Samia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Katibu wa Idara ya Oganaizesheni wa CCM, Maudline Cyrus Castico.
Mbali ya Rais Samia, hafla hiyo ya kuapishwa Rais Hichilema imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kikanda.
Akizungumza baada ya kuapishwa leo, Rais huyo mpya wa Zambia Hakainde Hichilema ameahidi kuujenga upya uchumi wa nchi hiyo unaoyumba na kupunguza umaskini.
Hichilema mwenye umri wa miaka 59 pia ameapa kurejesha haki za binadamu na uhuru wa watu mambo ambayo yalikiukwa chini ya mtangulizi wake.
“Tutajenga uchumi wetu ili tuweze kuwaondoa watu wengi katika umaskini kuliko ilivyokuwa”, alisema Hichilema alipohutubia umati wa wafuasi wake wa chama cha United Party for National Development.
Katika jaribio lake la sita la kuwania urais safari hii Hichilema alimshinda Rais aliyekuwapo madarakani Edgar Lungu kwa kura karibu milioni moja.
Rais anayeondoka madarakani nchini Zambia Edgar Lungu alikiri kushindwa na kumpongeza mrithi wake ambaye pia ni hasimu wake wa muda mrefu Hakainde Hichilema kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi uliokuwa na upinzani mkali.
Lungu aliahidi kufuata sheria na kuhakikisha ubadilishanaji mamlaka wenye amani. Katika hotuba yake ya kwanza kwa nchi, Hakainde Hichilema kwa upande wake ameukosoa utawala unaoondoka nchini Zambia akiahidi kuleta demokrasia nchini humo.
Rais Hichilema amedai yeye pamoja na wafuasi wake walikuwa waathiriwa wa utawala aliouita wa kikatili na ameahidi kurejesha uhuru, amani na kuheshimiwa kwa haki za binadamu.
Rais Hichilema ambaye ametokana chama kilichokuwa cha upinzani cha United Party for National Development (UPND) ametwaa kiti hicho baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Zambia, kumtangaz tarehe 16 Agosti 2021 amemtangaza kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha Urais kwa kupata kura 2,810,777.
Kufuatia kujizolea kura hizo Hichilema akawa amemshinda Edgar Lungu, Rais anayemaliza muda wake kutoka katika chama kilichokuwa kinatawala Zambia, cha Patriotic Front (PF) ambaye alipata kura 1,814,201.
Kinyang’anyiro cha Urais nchini Zambia, kiliwashirikisha wagombea 16 katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika, Jumapili tarehe 8 Agosti 2021 ambapo Wananchi milioni 7 nchini Zambia walikuwa wamejiandikisha kupiga kura kati ya wakazi milioni 19.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇