Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki y NMB, Ruth Zaipuna na Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi wakionyesha mkataba wa maelewano baada ya kutiliana saini mkataba wa maelewano wa mbio za NMB Marathon zenye lengo la kuchangia bilioni mmoja ndani ya miaka minne kwa ajili ya kuwatibu akinamama wenye Fistula. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa UAP Insurance, Nelson Rwihula na kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Sanlam Life Insurance, Julius Magabe.
Benki ya NMB, imesaini makubaliano
ya ushirikiano na Hospitali ya CCBRT, yanayolenga kukusanya kiasi cha Sh.
Bilioni 1 za matibabu ya Fistula kwa kina mama wasio na uwezo, kupitia Mbio za
Hisani za NMB Marathon, zitakazofanyika kwa mara ya kwanza Septemba 18, 2021
jijini Dar es Salaam.
Kupitia mbio hizo ambazo mwaka huu
zitafanyika chini ya kaulimbiu ya: 'Mwendo wa Upendo,' Benki ya NMB na CCBRT
wanatarajia kukusanya zaidi ya Sh. Milioni 250 kila mwaka kwa miaka minne ambazo
zitasaidia matibabu ya wagonjwa wa fistula, miongoni mwa mamia ya kina mama
wanaoteseka kwa maradhi hayo.
Akizungumza wakati wa utilianaji
saini wa makubaliano hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alibainisha
kuwa, Fistula ni maradhi yanayotesa kina mama wengi nchini, na akawataka
Watanzania kujitokeza kwa wingi kujisajili kushiriki mbio hizo, ili kufanikisha
lengo la kukusanya fedha ya matibabu ya wagonjwa hao.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji
Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi, alisema taasisi yake inajisikia faraja kubwa
kufanikisha utilianaji saini wa makubaliano hayo, sambamba na uzinduzi wa NMB
Marathon 2021, huku akieleza kuwa mashindano hayo yana maana kubwa kwa maelfu
ya kina mama wa Kitanzania.
NMB Marathon zitakuwa na sehemu
tatu ambazo ni mbio za kilomita 21 (nusu marathon), kilomita 10 na kilomita 5,
ambako washindi wa kwanza hadi wa 10 watapata medali na fedha taslimu.
Kwa mujibu wa Mratibu wa NMB
Marathon 2021, David Marealle, ada ya kujisajili kushiriki mbio hizo ni Sh.
30,000 kwa kilomita 21 na Sh. 20,000 kwa mbio za kilomita 10 na kilomita 5.
Washindi wa mbio za kilomita 21
wanaume na wanawake watajinyakulia Medali ya Dhahabu na fedha taslimu Sh.
1,400,000, huku washindi wa pili wakitarajiwa kutwaa Medali za Fedha na Sh.
1,100,000, wakati washindi wa tatu wakitengewa Sh. 700,000 na Medali za Shaba.
Huku kwa mbio za kilomita kumi,
700,000 na medali ya dhahabu, 500,000 na medali ya fedha pamoja na 300,000 na
medali ya Shaba kwa mshindi wa kwanza, pili na tatu kwa wanaume na wanawake.
Katika mbio za kilomita 5,
washindi upande wa wanawake na wanaume watajipoza na Medali za dhahabu na Sh.
250,000, washindi wa pili medali za fedha na Sh. 150,000, huku washindi wa tatu
wakiambulia medali za shaba na Sh. 100,000 taslimu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇