Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (aliyevaa koti la blue) akipata maelezo kutoka kwa Mkandarasi anayejenga barabara ya Lusitu – Mawengi (km 50) Mhandisi Dr Moon kwa kiwango cha zege la saruji wakati alipokagua maendeleo ya mradi huo, mkoani Njombe.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (aliyevaa koti la blue) akizungumza na wananchi wa Ludewa mara baada ya kukutana nao wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Lusitu – Mawengi (km 50) kwa kiwango cha zege la saruji, mkoani Njombe.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (aliyevaa koti la blue) akitizama namna ya zege la saruji linavyowekwa katika barabara ya Lusitu – Mawengi (km 50) inayoendelea kujengwa mkoani Njombe.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe Mhandisi Ruth Shalua, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa barabara Lusitu – Mawengi (km 50) kwa kiwango cha zege la saruji.
Muonekano wa hatua za ujenzi wa Daraja la Ruhuhu lenye urefu wa mita 98.7 ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 90. Daraja hilo litakapokamilika litafungua shughuli za usafirishaji katika mkoa wa Njombe na Ruvuma.
Mbunge wa jimbo la Ludewa, Joseph Kamonga, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipotembelea na kukagua bandari ya Manda, mkoani Njombe.
**************************
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewatoa hofu wananchi wa Kata ya Ruhuhu Wilaya ya Ludewa ambao wamekuwa wakiulalamikia ujenzi wa Daraja la Mto Ruhuhu ambao umechukua muda mrefu kukamilika kwake.
Mhandisi Kasekenya ameyasema hayo mkoani Njombe mara baada ya msafara wake kusimamishwa na wananchi wa kata hiyo na kuelezwa kero na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi.
“Hili daraja ni la muda mrefu tangu mwaka 2016 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alikwisha pita hapa na kuona adha na kero mnazozipata na alitoa ahadi kuwa lazima daraja hili likamilike na ndio maana tuko hapa kukamilisha ahadi hiyo”, amesema Naibu Waziri Kasekenya.
Aidha, amewaagiza Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe na Ruvuma kuhakikisha ndani ya wiki mbili kuanzia sasa vifaa vya ujenzi wa juu ya daraja vilivyopo Bandari ya Dar es Salaam vifike eneo hilo na kuanza kufungwa ili wananchi wa kata hizi waanze kutumia daraja.
Naibu Waziri Kasekenya ametoa wito kwa wananchi kulilinda daraja hilo ambalo linagharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.1 pindi litakapokamilika kwani linajengwa kwa fedha za Serikali kupitia kodi za wananchi.
“Kawaida daraja linapokamilika wananchi wanaanza kuchimba mchanga, kuiba vyuma vya daraja na kupitisha mifugo mahali pasipotakiwa, hivyo niwaombe wananchi mlilinde sana daraja hili”, amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya amekagua ujenzi wa barabara ya Itoni – Ludewa – Manda (km 211.4) sehemu ya Lusitu – Mawengi (km 50) kwa kiwango cha zege ambao unatekelezwa na Mkandarasi Cheon Kwang Engineering Costruction na ujenzi wake umefikia asilimia 69.
“Tunaendelea kumshukuru na kumpongeza Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea tena kwa kasi,” amefafanua Naibu Waziri Kasekenya.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hii ya Itoni – Ludewa – Manda kutafungua fursa za kiuchumi kwa mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla kwani maeneo hayo ndipo yanapopatikana kwa wingi makaa ya mawe na chuma cha liganga.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Njombe Mhandisi Ruth Shalua, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa kazi zilizofanyika mpaka sasa ni ujenzi wa tabaka la zege kwa kilometa 30, ujenzi wa makalvati makubwa 11 na makalvati madogo 96 kati ya 107 yamekamilika na kazi zingine zinaendelea.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Joseph Kamonga amemshukuru Naibu Waziri kasekenya kwa kuweza kukagua na kutembelea miradi iliyopo jimboni kwake na pia ameishukuru Serikali chini Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo mkoani Njombe kwa wakati na wakandarasi wote wapo maeneo yao ya kazi.
Imetolewa na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇