Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Gilbert Kalima, ameahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa bidii, uamiifu na weledi kadri awezavyo huku akizingatia Katiba, kanuni na taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Jumuiya hiyo katika kuleta maendeleo chanya kwa manufaa ya Jumuiya na Chama,
Kalima ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Kamat Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, amesema hayo leo, wakati akikabidhiwa rasmi Ofisi na Katibu Mkuu anayeondoka Erasto Sima, katika hafla iliyofanyika kwenye Ofisi za Jumuiya hiyo, Makao Makuu ya CCM, jijini Dodoma, na kuhudhiriwa na viongozi mbalimbali wa Jumuiya hiyo.
"Nashukuru kwa kukaribishwa siku ya leo katika ofisi hii, ninafahamu changamoto ni nyingi katika Jumuiya yetu lakini naamini kwa umoja wetu tukishirikiana tutavuka viunzi vyote vinavyotukabiri, sisi ni wazazi ndio tegemeo la busara kubwa kwa chama chetu.
Tujifunge mkanda kwa pamoja kazi iendelee kwa kushirikiana na chama chetu pamoja Jumuiya nyingine za Chama katika kuhakikisha tunatimiza lengo la ilani ya CCM ya mwaka 2020 - 2025 chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan", akasema Kalima na kuongeza:-
"Naomba pia nitumie fursa hii kukupongeza Nugu Sima kwa kuitumikia Jumuiya hii kwa juhudi na maarifa yako yote, hadi leo hii unaponikabidhi kijiti cha uongozi huku ukiiacha Jumuiya ikiwa imara katika nyanja nyingi", alisema Kalima.
Mapema, akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Katibu Mkuu anayeondoka wa Jumuiya hhiyo Sima, alisema anashukuru kwa kupata nafasi ya kuitumikia nafasi hiyo na kwamba kuna mambo kadhaa ya kiofisi na kijamii ambayo ameyafanya nchi nzima na kumuomba Katibu mkuu mpya kuyaendeleza yale mema.
Sima amewaomba Wafanyakazi wa Jumuiya hiyo katika ngazi zote kumpa ushirikiano Katibu Mkuu mpya kama ule waliokuwa wakimpa yeye wakati wa utumishi wake.
"Binafsi kwa niaba ya familia yangu ninakishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kuniamini na kunikabidhi nafasi hii ya Ukatibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi tangu mwaka 2018 hadi mwaka huu wa 2021, hivyo nisipokuwa na shukrani kwa nafasi hii nitakuwa sina shukurani, nawe Katibu Mkuu mpya nakupongeza kwa dhati kwa kuaminiwa kushika nafasi hii na ninakutakia kazi njema" alisema Sima.
Habari Picha👇
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Erasto Sima (kushoto), akimkabidhi vitendea kazi Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya hiyo Gilbert Kalima, wakati wa hafla ya makabidhano rasmi ya Ofisi yaliyofanyika leo katika Ofisi za Jumuiya ya Wazazi, Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma, leo.Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Erasto Sima, akizungumza, wakati wa hafla ya makabidhano rasmi ya Ofisi yaliyofanyika leo katika Ofisi za Jumuiya ya Wazazi, Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma, leo. Kushoto ni Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya hiyo Gilbert Kalima. (Na Mpigapicha Maalum)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇