Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani (kushoto) akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakati akizindua mradi wa usambazaji umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa mkoa huo uliofanyika wilyani humo, Agosti 01, 2021.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakifurahia jambo, wakati Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) akizungumza kabla ya kuzindua Mradi wa usambazaji Umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa Mkoa huo uliofanyika wilayani humo, Agosti 01, 2021.
Baadhi wa Vijana wa Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani)wakati akizindua Mradi wa usambazaji Umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa mkoa wa Ruvuma uliofanyika wilayani humo, Agosti 01, 2021.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Balozi Brigedia Generali Wilbert Ibuge (kulia) akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakati wa uzinduzi wa Mradi wa usambazaji Umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa mkoa wa Ruvuma uliofanyika wilayani humo, Agosti 01, 2021.
Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani(tatu kushoto) akiweka Jiwe la Msingi katika Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakati akizindua Mradi wa usambazaji Umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa Mkoa huo, uliofanyika wilayani humo, Agosti 01, 2021.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani)wakati akizindua Mradi wa usambazaji Umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa Mkoani humo uliofanyika wilayani humo, Agosti 01, 2021.
Na Zuena Msuya, Ruvuma
Imeelezwa kuwa shilingi Bilioni 71.95 zitatumika kutekeleza mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), Mzunguko wa Pili katika vijiji vyote ambavyo havijapekelewa umeme mkoani Ruvuma.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani wakati akizindua mradi huo kwa Mkoa wa Ruvuma,ambapo uzinduzi huo ulifanyika katika Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani humo Agosti 01, 2021.
Dkt. Kalemani alisema kuwa fedha hizo zitatumika kufikisha na kusambaza umeme katika Vijiji 265 vilivyobakia katika mkoa huo wenye jumla ya vijiji 554, ambapo tayari vijiji 289 vimeshafikiwa na umeme.
“Wanaruvuma hasa Tunduru tulipozindua mradi huu hakikisheni mnautumia umeme huu ipasavyo kwa kujiletea maendeleo pia anzisheni viwanda, Rais wa awamu ya Sita, Samia Suluhu Hasan ametoa fedha za kutosha kuhakikisha vijijini vyote vinapata umeme ifikapo Desemba 2022, sasa kazi kwenu kuandaa nyumba zenu na kwa sasa umeme ni lazima sababu Serikali imegharamia kila kitu, ninyi mtalipia shilingi 27,000 tu, hivyo msichezee nafasi hii, pia ni marufuku kununua nguzo” alisema Dkt. Kalemani.
Alifafanua kuwa kampuni mbili za kitanzania zimepewa dhamana ya kutekeleza mradi huo katika wilaya zote za mkoa husika ambazo ni Songea, Mbinga, Tunduru, Nyasa na Namtumbo,ambapo kazi hiyo imegawanywa katika makundi mawili.
Wakandarasi hao ni Kampuni ya NAMIS itayotekeleza mradi huo katika Wilaya za Songea, Mbinga na Nyasa kwa gharama ya TZS. Bilioni 35.281, na White City itatekeleza katika Wilaya za Tunduru na Namtumbo kwa gharama ya Bilioni 36.678.
Akizungumzia wilaya ya Tunduru ambapo ndipo mradi huo umezinduliwa kimkoa, Dkt. Kalemani alisema kuwa wilaya hiyo ina jumla ya vijiji 157, kati ya hivyo vijiji vyenye umeme ni 72 na visivyo na umeme ni 85.
Vijiji hivyo 85 vilivyosalia vitapelekewa umeme kupitia mradi huo uliozindiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 21.7 ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 12.
Kwa wilaya hiyo ya umeme utaanza kupelekwa katika kata ya Nalasi ikihusisa vijiji,vitongoji na mitaa vyote vya kata hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Balozi Brigedia Generali Wilbert Ibuge aliwataka wakazi wa mkoa huo kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme pamoja na kutoa ushirikiano kwa wakandarasi watakaotekeleza mradi huo.
Balozi Ibuge aliwataka vijana wa maeneo husika kuchangamkia fursa ya kufanya kazi zisizo na taaluma maalum, ili kuweza kujipatia kipato na kunufaika na mradi huo.
Hata hivyo aliwataka wakandasi waliopewa dhamana ya kutekeleza mradi hou kujitambulisha katika ofisi za serikali za mitaa, wakati wa kutekeleza miradi hiyo ili kupata ushirikiano zaidi na kurahisisha utendaji kazi wao.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇