Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Phillis Nyimbi amewafunda Mabinti nchini ili wafunguke na kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amewafunda kuwa kwa kufanya hivyo kila Binti hapa nchini ataweza kufikia kwa namna moja au nyingine ndoto zake za mafanikio ya kiuchumi, kijamii na hata kisiasa.
Dk. Nyimbi amewafunda Mabinti hao wakati akifungua Kongamano la Mabinti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) lililoitwa 'Naifikiaje Ndoto Yangu, Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii, lililoandaliwa na UWT Mkoa wa Dar es Salaam na kufanyika katika Ukumbi wa Karimjee.
Alisema Mabinti nchini hasa wale wa CCM hawana sababu ya kujikunyata na kuwa tegemezi kwa kuwa Serikali ya CCM inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama, Rais Samia imefungua fursa lukuki ambazo haziwabagui zinazopatikana katika miradi mingi ya Kimkakati inayotekelezwa nchini.
Alisema Rais Samia, katika kutekeleza dhamira yake ya kuhakikisha maisha ya wananchi wakiwemo mabinti yanakuwa bora, ameendelea kutiririsha fedha katika miradi hiyo ya kimkakati, hivyo sasa ni wajibu wa kila mwananchi kuchangamkia fursa hiyo.
“Sote tunajua Rais alitoa Sh. Milioni 500 kwa kila Jimbo ili kuboresha miundombinu ya barabara, ili ikurahisishie binti wa CCM, unapoenda shule uende kwa amani. Pia kwa kutumia barabara hizo uone fursa zingine za kujiinua kiuchumi,” alifafanua Katibu Mkuu huyo.
Alitaja moja ya mradi ambao mabinti wa Tanzania wanaweza kunufaika na fursa zilizopo kuwa ni Daraja la Selender “Tanzanite’ jijini Dar es Salaam, linalokatiza baharini kati ya Ufukwe wa Aga Khan hadi ufukwe wa Coco Beachi linalojengwa kwa sh. Bilioni 243.75.
“Swali langu kwenu mabinti wa CCM pale kwenye Daraja la Tanzanite, daraja la kihistoria, ambalo linaweza kuifanya Tanzania, kusababisha watu kuja ili kuangalia wewe umejipangaje na hiyo fursa?” alihoji Dk. Nyimbi na kuingeza kuwafunda Mabinti hao kuwa kwa kuwahoji;
“Hivi hadi sasa yupo hata Binti mmoja wa CCM aliyeenda katika Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utali Dk. Damas Ndumbalo kwenda kuuliza kuna fursa gani za utalii, ili achukue zile fursa akazifanyie kazi daraja lile litakapokamilika ?”
Alisema , pia Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayojengwa nao unafursa nyingi kwa mabinti kwa kuwa licha ya kurahisisha usafiri na kuokoa muda lakini utapanua fursa ya kukuza uchumi kwa namna mbalimbali kutegemea na fursa ambayo mtu ataamua kuishika mradi huo ukianza.
“Lakini je, kwenye lile li-treni yupo binti yeyote wa CCM anayefikiria kuja kuwa dereva wa matreni yanayotembea kwa umeme? Au tunasubiri kaka zetu waendelee kuwa madereva?.
Kwa nini wewe binti usiwe dereva wa kwanza katika chi yetu ya Tanzania ukaendesha treni hiyo ya umeme? Pale kuna fursa ya madereva. Pia kuna fursa ya kutengeneza vichwa vya matreni hayo na mabehewa,”alisema Dk. Nyimbi.
Aliwachagiza mabinti kusomea uhandisi wa ufundi mitambo, ili kuziba mwanya wa fursa hiyo kwenda kwa mafundi watakaotafutwa mbali nje ya Nchi.
Alibainisha kuwa serikali chini ya Rais Samia, imeboresha miundombinu ya elimu ikiwemo kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kufikia sh. bilioni 500.
“Lakini kama haitoshi serikali ya CCM imeendelea kuelekeza Halmashauri zote nchini zitenge asilimia 10 ya mapato yake ya ndani, asilimia nne kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.
Sasa fursa ya mikopo hii ambayo haina riba ni lazima muichangamkie maana mnazo sifa za kunufaika kwa kuingia katika makundi yote hayo matatu maana nina uhakika hata upande wa walemavu mabinti wamo.
Awali Mwenyekiti wa UWT wa MKoa wa Dar es Salaam, Florance Masunga, alisema, kongamano hilo ni hatua kubwa ya kumwandaa binti kushiriki katika ujenzi wa taifa kwa kutambua fursa zilizo kupitia Jumuia hiyo na CCM.
“Kongamano hili ni la pili na litafuata kongamano kwa wanawake wenye ulemavu 200 na la wajane 200,”alibainisha.
Mwanasiasa mkongwe Getrude Mongela na Waziri na Mbunge wa zamani Profesa Anna Tibaijuka ni miongoni mwa waliotoa mada kwenye kongamano hilo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Dk. Phillis Nyimbi akizungumza wakati akizindua semina ya Mabinti wa CCM katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, leo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Dk. Phillis Nyimbi (Wapili kushoto), akisalimiana na viongozi wa Umoja huo mkoa wa Dar es Salaam, alipokuwa akiwasili katika viwanja vya Karimjee, kufungua semina ya Mabinti wa CCM. Kushoto ni Katibu wa UWT mkoa wa Dar es Salaam Grace Haule, Watatu ni Mwenyekiti wa UWT wa mkoa Florence Masunga na kushoto kwa Florence ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT mkoa wa Dar es Salaam, Mjumbe wa NEC na Mtumishi wa Vyombo vya Habari vya Chama Angel Akilimali.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Dk. Phillis Nyimbi akiingia ukumbini kwa shangwe na nderemo huku akifuatana na baadhi ya viongozi wa Umoja huo mkoa wa Dar es Salaam, alipowasili kufungua semina ya Mabinti wa CCM katika ukumbi wa Karimjee. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa UWT wa mkoa Florence Masunga.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Dk. Phillis Nyimbi (wapili kushoto) akicheza na viongozi wa meza kuu wimbo wa ' Wanawake na Maendeleo' uliotumbuizwa baada ya kuingia ukumbini. kufungua semina ya Mabinti wa CCM katika ukumbi wa Karimjee. Kushoto ni Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Dar es Salaam Florence Masunga na Watatu kushoto ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT mkoa wa Dar es Salaam, Mjumbe wa NEC na Mtumishi wa Vyombo vya Habari vya Chama Angel Akilimali na kulia ni Waziri na Mbunge mstaafu Prof. Anna Tibaijuka.
Katibu wa UWT mkoa wa Dar es Salaam Grace Haule akimkaribisha mgeni rasmi ukumbini na kufanya utambilisho wa wageni waalikwa.
Katibu wa UWT mkoa wa Dar es Salaam Grace Haule akisoma risala kwa mgeni rasmi.
Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Dar es Salaam Florence Masunga akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuzungumza.
Mwanasiasa mkongwe na mwanaharakati aliyebobea hasa katika utetezi wa haki za wanawake Getrude Mongela akitoa mada wakati wa Semina hiyo.
Waziri na Mbunge mstaafu Prof. Anna Tibaijuka akitoa mada wakati wa semina hiyo.
Mwisho wa shughuli ikawa picha ya pamoja na viongozi.
©2021Official CCM Blog/Bashir Nkoromo
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇