Kihongosi (kulia) akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo.PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA
Na Richard Mwaikenda, CCM Blog, Dodoma
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umelaani na kupinga vikali kauli za baadhi ya viongozi wa chama na serikali wanaotoa maneno yasiyofaa na ya kichochezi kuhusu chanjo.
Tamko hilo limetolewa leo Julai 27, 2021 na Katibu wa UVCCM, Kenani Kihongosi alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma, ambapo amekitaka chama kuwachukulia hatua kali za kinidhamu.
Kihongosi hakusita kumtaja mmoja wa viongozi hao kuwa ni Mbunge wa Jimbo la Kawe, Askofu Josephat Gwajima kwa madai ametoa maneno yasiyofaa kuhusu chanjo alipokuwa akihubiri juzi katika Kanisa lake la jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa laitiMbunge huyo angekuwa na jambo angefuata utaratibu wa kwenda kuongea kwenye vikao maalumu vya chama kuliko kuongea hadharani kuwashawishi wananchi wasiende kuchanjwa akidai chanjo ilioyoingizwa nchini haifai, kitendo ambacho ni ukiukwaji wa taratibu za kichama na kumvunjia heshima Mwenyekiti wa Chama Cha Cha Mapinduzi,Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ametangaza wazi kuwa chanjo ni hiari.
"Juzi tumesikia Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima akihubiri kanisani kwa maneno yasiyofaa na ya kichochezi kwa kuwagawa wananchi kwa kuwataka wasiende kupata chanjo akisema haifai, wakati tayari msimamo umeshatolewa na serikali pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kwamba inafaa na ni hiari ya mtu kuchanjwa," amesema kihongosi.
Pia, kiongozi huyo wa Umoja wa Vijana wa CCM, ametoa rai kwa viongozi wa chama na serikali pamoja na watu wengine wanaotoa maneno yasiyofaa wanaohamasisha watu wasiende kuchanjwa licha ya serikali kutoa msimamo wake kuacha tabia hiyo.
Amesema kuwa Uvccm inasimama na serikali na rais, hasa kuhusu suala la chanjo na kuwataka wananchi wasiogope kwenda kupata chanjo ambayo inazinduliwa na Rais Samia kesho Julai 28,2021 Ikulu Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇