Meneja Msaidizo wa Idara ya Mawasiliano ya BoT, Victoria Msina akizungumza maneno ya utangulizi wakati wa mkutano huo.
Baadhi ya maofisa wa BoT |
Waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini wakato Gavana Luoga akizungumza.
TAARIFA YA BOT KWA UMMA
Hatua za kisera kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi na kupunguza viwango vya riba
Janga la UVIKO-19 limeathiri shughuli za
kiuchumi, kutokana na nchi zinazofanya biashara na Tanzania kuchukua hatua kudhibiti
kuenea kwa UVIKO-19, ikiwemo vizuizi vya kusafiri. Kwa sababu hiyo, Serikali
imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kupunguza athari za janga hilo katika
shughuli za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa uchumi. Pamoja na hatua hizo, kasi
ya ukuaji ilipungua hadi kufikia asilimia 4.8 mwaka 2020 kutoka asilimia 7 kwa mwaka
uliotangulia. Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi pia ulipungua, kufikia ukuaji
wa kati ya asilimia 2.3 hadi asilimia 9.1. Viwango vya riba kwa mikopo
inayotozwa na benki za biashara vimeendelea kuwa juu, kwa wastani wa asilimia
17, licha ya ongezeko la ukwasi na hatua zingine zilizochukuliwa.
Ili kutoa msukumo mkubwa wa kuongeza kasi
ya mikopo kwa sekta binafsi na kupunguza riba, na hivyo kuchochea kasi ya
ukuaji wa uchumi, Benki Kuu ya Tanzania imeamua kutekeleza hatua za kisera
zifuatazo, kuanzia tarehe 27 Julai 2021:
(i)
Kupunguza
kiwango cha sehemu ya amana za mabenki kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu
(Reduction of statutory minimum reserve
requirement-SMR). Benki Kuu imetoa
unafuu kwa benki za biashara kwa kupunguza kiwango cha kisheria cha amana
ambacho benki na taasisi za fedha zinatakiwa kuweka Benki Kuu, ikiwa ni sehemu
ya kutekeleza sera ya fedha. Nafuu hii itatolewa kwa benki itakayotoa mikopo
kwa sekta ya kilimo kulingana na kiasi cha mkopo kitakachotolewa. Aidha, benki
itakayonufaika itatakiwa kutoa mikopo kwa sekta ya kilimo kwa riba isiyozidi
asilimia 10 kwa mwaka. Hatua hii inalenga kuongeza mikopo katika sekta ya
kilimo,na kupunguza riba katika mikopo itakayotolewa.
(ii)
Kulegeza
masharti ya usajili wa mawakala wa benki (relaxation of agent banking eligibility
criteria). Benki Kuu ya Tanzania imeondoa sharti la uzoefu wa kufanya biashara kwa angalau
miezi 18 kwa waombaji wa biashara ya wakala wa benki. Badala yake, waombaji wa
biashara ya wakala wa benki watatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa au Namba
ya Kitambulisho cha Taifa. Hatua hii itachangia
kuongeza fedha katika mabenki kutokana na ongezeko la amana na kupunguza riba
za mikopo.
(iii) Ukomo wa riba
kwenye akaunti za makampuni ya watoa huduma za fedha kwa njia ya simu za
mkononi (Limitation of interest rate paid on mobile money trust accounts).
Benki Kuu imeweka ukomo wa
kiwango cha riba kinachotolewa na benki za biashara kwenye akaunti za makampuni
yanayotoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi. Riba itakayotolewa
kwenye akaunti hizi haitazidi riba itolewayo na benki husika katika amana za
akiba (savings deposit rate). Hatua hii inalenga kupunguza gharama za
upatikanaji wa fedha kwa benki zinazotumika kukopesha, hivyo kuchangia
kupunguza riba za mikopo.
(iv) Kuanzishwa
kwa mfuko maalum wa kukopesha mabenki na taasisi za fedha ili ziweze kukopesha
sekta binafsi. Benki Kuu imeanzisha mfuko maalum wenye
thamani ya shilingi trilioni moja ambao utatumika kukopesha mabenki na taasisi
za fedha kwa riba ya asilimia 3, ili taasisi hizo ziweze kukopesha sekta binafsi.
Benki au taasisi ya fedha itakayofaidika na mfuko huu itatakiwa kukopesha sekta
binafsi kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka. Hatua hii itaongeza ukwasi na
kupunguza riba za mikopo kwa sekta binafsi.
(v) Kupunguza kiwango cha mtaji
kinachotakiwa kuwekwa na benki za biashara kwa ajili ya kuweza kutoa mikopo (Reduction of risk weight on loans). Benki
Kuu imepunguza kiwango cha mtaji kinachotakiwa kuwekwa na benki za biashara kwa
ajili ya kuweza kutoa mikopo. Hatua hii itasaidia kutoa fursa kwa benki za
biashara kutoa mikopo zaidi kwa sekta binafsi kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Hatua hizi za kisera zimechukuliwa
kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura. 197 na Sheria ya Mifumo ya
Malipo ya Taifa, Sura ya 437. Benki Kuu itatoa mwongozo wa namna ya utekelezaji
wa hatua hizi kwa benki, taasisi za fedha na makampuni yanayotoa huduma za
fedha kwa njia ya simu za mkononi. Pamoja na hatua hizi, Benki Kuu inaziagiza
benki za biashara na taasisi za fedha kuweka na kutekeleza mikakati ya
kupunguza riba za mikopo na kuhamasisha upatikanaji wa amana.
Prof. Florens
D.A.M Luoga
Gavana
BENKI
KUU YA TANZANIA
27 Julai 2021
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇