Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga akikagua maendeleo ya ujenzi wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA Wilaya ya Kwimba.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga akitoa maelekezo kwa fundi na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA Wilaya ya Kwimba.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga akiongea na baadhi ya watumishi wa VETA, Wizara ya Elimu na wananchi wa Wilaya ya Kwimba wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA cha Wilaya ya Kwimba.
Baadhi ya watumishi wa VETA, Wizara ya Elimu na wananchi wa Wilaya ya Kwimba wakifatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga (hayupo pichani) wakati akizungumza nao mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA cha Wilaya ya Kwimba.
………………………………………………………………………….
Na WyEST
Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 48.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyuo 29 vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) vya Wilaya kikiwemo chuo cha Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza ambacho kinatarajiwa kukamilika Septemba 30 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa Chuo hicho ambapo amesema fedha za kukamilisha ujenzi wa chuo hicho tayari zimeshatengwa ili kuhakikisha kinamilika kwa wakati uliopangwa na kwamba mafunzo yataanza mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.
Amesema gharama za ujenzi wa chuo hicho mpaka kukamilika utatumia zaidi ya Shilingi bilioni 2.1 na kwamba hadi sasa imeshatumika Bilioni 1.6 huku Shilingi milioni 500 iiliyobaki ikiwa imetengwa katika mwaka wa fedha 2021/22 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo hicho.
“Niwatoe wasiwasi wananchi wa Kwimba kuwa ujenzi huu unakwenda kukamilika kama ulivyopangwa na tutaanza na kozi za muda mfupi kisha Januari mwakani tutaanza kutoa kozi za muda mrefu,” amesema Mhe. Kipanga.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kagera, Juliana Magesa ambaye ndiye msimamizi mkuu wa mradi huo amesema mradi una jumla ya majengo 17 yakiwemo mabweni mawili yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 144, kati yao 80 wa kiume na 64 wakike.
Amesema mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 62 na inatarajiwa hadi ifikapo Septemba 30 mwaka huu ujenzi huo utakuwa umekamilika ili kutoa fursa kwa vijana wa Wilaya ya Kwimba na maeneo jirani kupata stadi za kazi watakazozitumia kujiajiri na kuajiriwa na hivyo kukuza uchumi wa Wilaya na Taifa kwa ujumla.
Akiongea kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Kwimba, Mbunge wa Wilaya hiyo, Mansoor Shanif ameishukuru Wizara ya Elimu kwa kujibu ndoto ya muda mrefu ya wananchi wa Kwimba ambayo sasa wanaona inaenda kutimia. Aidha, ameomba Wizara kujenga uzio wa kuzunguka chuo hicho ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mwingiliano.
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Kwimba Nyakia Ally, ameshukuru Wizara kwa ujenzi wa chuo hicho cha ufundi na ameshauri kiwe na mafunzo ya ufundi magari pia ili kuwarahisishia wananchi wa Kwimba ambao huwa inawabidi waende Mwanza mjini ambapo ni umbali wa kilometa 97 ili kupata mafundi wa kutengeneza magari yao.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇