LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 6, 2021

RAIS SAMIA AMUALIKA RAIS WA MAREKANI JOE BIDEN KUTEMBELEA TANZANIA

 

Rais wa Marekani Joe Biden


Leo, Julai 6, 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa mwaliko kwa  Rais wa Marekani Joseph Biden  kutembelea Tanzania ili kuzidi kuimarisha uhusino uliopo kati ya nchi hizi mbili. 


Mwaliko huo ni miongoni mwa mambo ambayo Rais Samia ameyasema,  wakati akizungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, akiwa Ikulu jijini Dodoma, leo.


Taarifa iliyotolewa jioni hii na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu imesema katika mazungumzo hao Rais Samia ameshukuru Waziri huyo kwa pongezi alizompa kwa kushika hatamu ya uongozi wa Tanzania.


Kwa mujibu wa Taarifa hiyo Rais Samia ameahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya  Marekani kukuza uhusiano baina ya nchi hizi mbili katika majukwaa mbalimbali ya Kimataifa. 


Mapema  Waziri Blinken alitangulia kumpongeza Rais Samia kwa kushika hatamu ys Uongozi wa nchi na kumhakikishia kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuleta maendeleo kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa kuzingatia vipaumbele vya nchi.


Katika mazungumzo hayo, pia Waziri Blinken amepongeza Rais Samia kwa hatua anazozichukua katika kukabiliana na ugonjwa  wa Corona nchini Tanzania na Marekani ipo tayari kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa huo.


Aidha, Blinken amepongeza  jitihada za Rais Samia katika kuimarisha Demokrasia nchini ikiwa ni pamoja na azma yake ya kukutana na kushirikiana na Vyama vya Siasa  pamoja na kusimamia  Uhuru wa Vyombo vya Habari.


Pia amepongeza uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na kuahidi kuwa hali hiyo imeivutia Marekani kushawishi wawekazaji wake kuja kuwekeza nchini. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwa njia ya Simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani  Antony Blinken, akiwa Ikulu Jijini Dodoma, leo. (Picha na Ikulu).

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages