Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza na wananchi wa Masasi alipokwenda kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo jana ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango alipofanya ziara katika mkoa wa Mtwara hivi karibuni.
Sehemu ya wananchi wa Masasi mkoani Mtwara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokwenda kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiwasikiliza baadhi ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya ya Masasi jana ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango alipofanya ziara katika mkoa wa Mtwara hivi karibuni.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara Rehema Mwinuka akizungumza katika mkutano wa hadhara wakati Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokwenda kusikiliza na kuipatia ufumbuzi migogoro ya ardhi katika wilaya ya Masasi mkoani Mtwara jana.
*******************************
Na Munir Shemweta, MASASI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesikiliza kilio cha wananchi wa wilaya ya Masasi kuhusiana na migogoro ya ardhi na na kumuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara Rehema Mwinuka kufuatilia utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Mtwara.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wakati wa kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi changamoto za sekta ya ardhi katika wilaya ya Masasi Julai 27, 2921 mkoani Mtwara, Dkt Mabula alisema katika ziara yake wilayani humo amebaini uonevu unaofanywa na baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi wasio waaminifu kutowatendea haki wananchi wakati wa kushughulikia changamoto za ardhi.
‘’Hapa nimegundua kuna jambo moja na nakuelekeza Kamishna wa Ardhi fuatilia katika halmashauri zako zote kuna uonevu mkubwa kwenye maeneo ya wananchi, kwa sababu hoja zote zinazoongelewa hapa ni shamba langu limechukuliwa sikupewa chochote au shamba langu ekari sita nimepewa kiwanja kimoja huu ni uonevu ambao serikali haiwezi kuvumilia’ alisema Dkt Mabula.
Wakiwasilisha malalamiko yao mbele ya Naibu Waziri Dkt Mabula, Wananchi wa Masasi mkoani Mtwara waliwatuhumu baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya hiyo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao na hivyo kuchangia kuwepo migogoro ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali.
Wananchi hao waliokuwa na jazba walieleza kuwa, baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi kwenye wilaya ya Masasi ni chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi kutokana na kutotekeleza majukumu ya kazi zo na wakati mwingine wameshindwa hata kufuata maelekezo ya viongozi.
Mkazi wa kata Mtandi Marambo Juu wilayani Masasi Bw. Patrick Kandulu alimtuhumu Mpima ardhi wa halmashauri kwa madai kuwa imekuwa ngumu kumpata afisa huyo kwa ajili ya kwenda uwandani na hivyo kukwamisha mara kadhaa zoezi lake la kupimiwa eneo lake.
Wananchi wengine walimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa, wamedhulumiwa maeneo yao na Halmashauri kwa kushindwa kuwalipa fidia ama kuwapa viwanja mbadala baada ya maeneo yao kuchukuliwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama vile ujenzi wa shule, maeneo ya wazi pamoja na barabara.
Dkt Mabula aligiza halmashauri zote kuhakikisha hazichukui maeneo ya wananchi bila ya kuwa na fedha za kuwalipa fidia na kumtaka mkurugenzi wa halmashauri ya Masasi kuwalipa fidia ama kuwapa viwanja mbadala wananchi wote ambao maeneo yao yamechukuliwa.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ambaye ilimlazimu kwenda uwandani kushuhudia na kutatua kero ya mwanamchi mmoja alisikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi zaidi ya 40 kwenye wilaya ya Masasi ikiwa ni maagizo ya Makamu wa Rais Dkt Philip Isdor Mpango aliyemtaka kwenda Wilayani humo kutatua migogoro ya ardhi iliyojitokeza wakati wa ziara yake mkoani Mtwara hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇