Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Mkoani
Manyara, Daniel Sillo akizungumza na wananchi wa Kata ya Ufana, kwenye
ziara yake ya kutembelea Kata zote 25 na kusikiliza kero na changamoto
zao na kuzungumza nao.
*************************
Na Mwandishi wetu, Babati
MBUNGE wa Jimbo
la Babati Vijijini Mkoani Manyara, Daniel Sillo ameahidi kutoa mabati
110 ili kukamilisha ujenzi wa shule shikizi ya msingi Datar iliyopo kata
ya Ufana.
Sillo amesema
mabati hayo atayatoa kutoka kwenye fedha za mfuko wa jimbo 2021/2022 ili
kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu na kuwapunguzia
msongamano.
Sillo ametembelea
shule hiyo ambayo ujenzi wake unaendelea ikiwa ni mwendelezo wa
kuzitembelea shule mbalimbali na kutoa misaada ambapo ameshatoa mifuko
ya saruji kwenye shule zilizopo jimboni kwake pamoja na mashine za
kutolea nakala (photo copy) kwa baadhi ya shule za Sekondari.
Amefanya ziara
kwa kata ya Secheda na Ufana ikiwa ni muendeleo wa ziara yake kwa kata
zote 25 zilizomo ndani ya Jimbo hilo katika kuwashukuru, kuwasikiliza
wananchi, kutatua kero zinazowakabili sambamba na kuwahamasiha juu ya
utendaji wa shughuli za kimaendeleo.
Katika ziara hiyo
Sillo ameambatana na viongozi wa CCM na wataalamu kutoka idara
mbalimbali ili kuweza kubainisha changamoto zinazowakabili wananchi na
kuzipatia majawabu ya papo kwa hapo.
Amewahimiza
wananchi wa kata hizo juu ya kuwa wamoja na kushirikiana katika kutatua
changamoto za kata hiyo na kuwataka kupokea fedha za maendeleo
zinazotolewa na serikali ili kuruhusu huduma za kijamii kuendelea.
“Maendeleo
yanatokana na ushirikiano wa viongozi na wananchi kwani yanaletwa kwa
pamoja na siyo vinginevyo hivyo wananchi wa jimbo la Babati Vijijini
tunapaswa kutambua hilo,” amesema Sillo.
Katibu wa Jumuiya
ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Babati Vijijini,
George Sanka amewataka viongozi wa vijiji kuwa sehemu ya utatuzi wa
migogoro mbalimbali katika maeneo yao.
Sanka amesema
viongozi wa vitongoji na vijiji wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika
kuleta maendeleo huku akisisitiza kuwepo na upendo, shirikiano, amani na
umoja Katika kuwatumikia wananchi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇