Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimkaribisha Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan wakati walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiteta jambo jambo na Balozi wa Finland nchini Mhe. Riitta Swan wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi wa Finland nchini Mhe. Riitta Swan akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati wa mazungumzo baina yao yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Maongezi baina ya Balozi wa Finland Mhe. Riitta Swan na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
**************************
Na Mwandishi wetu, Dar
Nchi ya Finland imeipongeza Tanzania kwa hatua mpya za kimaendeleo katika nyanja za ushirikishwaji wa sekta binafsi, uhuru wa vyombo vya habari,utawala bora na haki za binadamu pamoja na mapambano dhidi ya UVIKO 19.
Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan ametoa pongezi hizo wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Balozi Swan amesema uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kukuza sekta binafsi, uhuru wa vyombo vya habari, kutoa kipaumbele kwa masuala ya utawala bora na haki za binadamu ikiwemo suala la kujiunga na mpango wa chanjo dhidi ya UVIKO 19 ni hatua inayopaswa kupongezwa.
“……….pamoja na masuala mengine suala la Tanzania kukubali chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 ni maendeleo mazuri sana kwa Taifa hili,” amesema Balozi Swan
Balozi Swan pamoja na mambo mengine, amejadiliana na Balozi Mulamula masuala mbalimbali ya kuimarisha na kukuza ushirikiano baina ya Finland na Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema Tanzania na Finland zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu tangu Tanzania ilipopata Uhuru ambapo Finland imekuwa ikisaidia kukuza na kuendeleza sekta za kimaendeleo hususan Elimu, Afya, Utalii, Mazingira pamoja na Maliasili.
“Katika jitihada za kuendeleza ushirikiano wetu na Finland,imeandaa mpango mkakati wa maendeleo katika nyanja mbalimbali kama vile masuala ya misitu, utawala bora, haki za binadamu na masuala ya kuendeleza wanawake ambapo nimepokea rasimu ya mpango huo leo na nitaufanyia kazi ili tuweze kuendeleza ushirikiano wetu kwa maslahi ya mataifa yetu,” Amesema Balozi Mulamula
Balozi huyo wa Finland amekutana na Balozi Mulamula kwa lengo la kuwasilisha mpango mkakati wa miaka minne wa Finland katika nyanja za mashirikiano na Mataifa mengine ikiwemo kukuza na kuendeleza diplomasia ya uchumi kupitia biashara na uwekezaji.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇