Dotto Mwaibale, Singida.
MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Martha Gwau ametoa bima za afya kwa wanawake 400 mkoani hapa ili ziwasaidie kupata matibabu.
Gwau alitoa bima hizo jana wakati
akihutubia kwenye kongamano la wanawake Mkoa wa Singida lililofanyika Ukumbi wa
Chuo cha Utumishi wa Umma ambapo pamoja na mambo mengine walitafakari siku 100
za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwa madarakani na mafanikio ya wanawake hapa
nchini huku kauli mbiu ikiwa ni 'Wanawake ni Nguzo ya Maendeleo' Kazi
iendelee..
" Bima hizi ni zawadi ya Afya
kutoka katika mfuko wa ofisi yangu na nijuhudi za kumuunga mkono Rais wetu
Samia Suluhu Hassan katika kuboresha afya za akina mama kwani bila afya hakuna
maendeleo na ili maendeleo yaje na kufanya kazi kwa bidii ni budi kila mtu kuwa
na afya njema, hivyo nimeamua kugharamia suala la afya kupitia mfuko wa bima wa
CHF kwa wanawake hawa ambao ni sawa na kaya 400 huku wanufaika wakiwa 2400
pamoja na watu wenye uhitaji maalumu".alisema Gwau.
Alisema bima hiyo itakuwa ya watu
sita kutoka kwenye kila familia ya wanawake hao 400.
Gwau alisema mwaka huu ameanza na kaya 400
lakini matarajio yake ni kufikisha kaya 1000 na wanufaika wakiwa zaidi ya 5000
itakuwa vizuri zaidi na anafanya hivyo kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu
Hassan za kuwatumikia watanzania katika sekta ya afya.
Pia Gwau alisema kuanzia kesho atatoa
utaratibu kwenda kwenye halmashauri zao ambako anatoka kila mwanamke kwa ajili ya kujisajili ambapo wanatakiwa watu sita yaani
baba, mama na watoto wanne walio chini ya umri wa miaka 18.
Gwau alitumia kongamano hilo
kwa ajili ya kuwashukuru wanawake hao kwa kumchagua kwa kura nyingi na kuwaomba
ushirikiano ambapo pia alieleza mipango na mwelekeo wake wa kazi za maendeleo
mkoani Singida.
Alisema ataanza ziara zake za kikazi
katika wilaya zote na kata ili kwa pamoja waweze kutatua kero za wanawake huku
vipaumbele vyake vikiwa ni kuwainua wanawake kiuchumi na kuwapatia elimu na
mafunzo mbalimbali na kuijenga Jumuiya yao ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi
Tanzania (UWT)
Alisema katika masuala ya kuwasaidia
wanawake atakuwa akifanya kwa awamu kulingana na atakavyo jaliwa lakini ya
kiutendaji yatakuwa wilayani ambapo aliwaomba wamshike mkono, wamuelekeze,
wamshauri na kumkoasoa lengo likiwa ni kuijenga Singida.
Aidha Gwau aliwaomba wanawake hao kumuunga
mkono Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ni mwanamke wa kwanza hapa nchini kushika
wadhifa huo mkubwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa ambapo alisema kwa umoja wao
wanapaswa kuonesha mshikamano na jinsi walivyo tayari kufanya naye kazi akiwa
katika nafasi hiyo na kumuombea kwa Mungu.
Katika hatua nyingine aliwataka wanawake
hao kuchangamkia fursa ya kilimo cha alizeti kwa kuwa ndio zao kubwa la
biashara mkoani hapa na Serikali imeweka nguvu ya kulilima kwenye mikoa
mitatu ya Singida, Dodoma na Simiyu.
Pia aliwaomba madiwani wanawake
kusimamia na kuwashauri wanawake kuchangamkia mikopo kutoka katika halmashauri
zao kwaajili ya kujiletea maendeleo na kuinua uchumi wa mwanamke.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (
CCM) Mkoa wa Singida Alhaji Juma Kilimba ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye
kongamano hilo alimshukuru Gwau kwa kuandaa kongamano hilo na kuwashukuru
wanawake hao kwa kumchagua kuwa mbunge.
Aliwataka wanawake hao kuwa wamoja na
kushirikiana kwa kila jambo sambamba na kuimarisha jumuiya yao ili chama hicho
kiendelee kuongoza nchi.
Katika kongamano hilo Gwau aliwaalika wataalamu ambao walitoa mada kuhusu masuala ya afya hususani namna ya kujikinga na ugonjwa wa corona na umuhimu wa kujiunga na bima ya afya.
Jambo jema kwani Afya ninmsingi wa maendeleo. Big up Mbunge Martha
ReplyDelete