Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Da es Salaam Janeth Mahawanga akiwa katika Picha ya pamoja na Viongozi wa UWT mkoa huo.
Na CCM Blog, Dar es Salaam
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam Janeth Mahawanga ameahidi kutoa tani 25 za Saruji kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa nyumba za watumishi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Wilaya zote tano za Mkoa wa Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge huyo imesema Janeth ametoa ahadi hiyo alipohudhuria Kikao cha Kamati ya Utekelezaji Mkoa wa Dar es Salaam kilichohudhuriwa na Wabunge, Madiwani wa Viti Maalum, Wenyeviti na Makatibu wa Wilaya kilichofanyika Wilaya ya Kinondoni mapema mwezi huu.
"Maendeleo ya Mkoa wa Dar es Salaam yataletwa na sisi wenyewe, hivyo ni lazima tuonyeshe ushirikiano , umoja, upendo na mshikamano, sambamba na kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu ili UWT katika mkoa huu tuweze kuwa na miradi ya maendeleo na kuwaletea Wanawake mabadiliko ya kiuchumi", amesema Mbunge huyo wakati akitoa ahadi hiyo ya saruji.
Vilevile Mbunge Janeth Mahawanga alisisitiza kuwa atatoa ushirikiano sawa kwa asilimia 100 kwa Wilaya zote tano za mkoa huo na kuwaomba Viongozi hao wamtume kwani Kinamama wa Mkoa wa Dar es Salaam walimpa dhamana hiyo hivyo yupo kwenye kiti hicho kwa ajili ya kuwatumikia na atahakikisha anaitendea haki nafasi hiyo.
Aliupongeza sana Uongozi wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam ngazi zote Wilaya na Mkoa sambamba na Madiwani wote wa Viti Maalum kwa kuungana kwenye kampeni ya kuhakikisha kuanzia Mkoa mpaka Wilaya zote zinakuwa na nyumba za Watumishi na vitega uchumi vya Jumuiya.
"Hivyo naahidi kuchangia tani 25 za saruji kuhakikisha kampeni hii inafanikiwa kwa Wilaya zote tano za mkoa huu", alisema Mbunge Janeth Mahawanga..
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇