LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 31, 2021

DC IRAMBA AWATAKA WATUMISHI KUISHI KATIKA VITUO VYAO VYA KAZI

Na Hemedi Munga, IRAMBA

Jumamosi Julai 31, 2021

MKUU wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amemuagiza Afisa Elimu Kata ya Kisiriri Wilayani Iramba Mkoa wa Singida kuwaandikia barua Walimu wote wanaokaa nje ya kata hiyo wawe wamekwisha hamia katika vituo vyao vya kazi ifikapo Agasti 10, mwaka huu.


Mwenda ametoa agizo hilo  mwishoni mwa juma hili,  wakati akiwa katika ziara yake ya kusikiliza kero na kuzitatua katika kata ya Kisiriri Wilayani hapa.


“Kuanzia leo hii nimeagiza Walimu wote waishi katika kata hii, ambaye hawezi kuishi hapa kijijini atuandikie barua kuwa kazi imemshinda, sisi tutatafuta walimu wengine maana kuna vijana wengi sana wanamaliza vyuo vikuu wanahitaji kazi mahali popote.” Aliagiza Mkuu huyo wa Wilaya.


Katika hatua nyingine, Mwenda amewataka wananchi kukata kadi ya CHF ili wasitozwe tena fedha yoyote wanapokuwa wamekwenda hospitali, kituo cha Afya au Zahanati.


“Ndugu zangu wananchi hakuna utaratibu wa mtu anayekua na kadi ya CHF kutakiwa kutoa tena shilingi elfu kumi anapokwenda Zahanati au hospitali ya Wilaya.” Alisema Mwenda na kuongeza kuwa


“Tukubaliane kuwa wananchi hawa wakate kadi za CHF halafu waone faida ya kuwa na kadi ya CHF pale watakapoumwa wanapata dawa itawafanya wahamasishane wao kwa wao kukata kadi ya CHF na kila mmoja atakua na kadi kwa kuwa anahitaji huduma ya matibabu na anayapata.”


Aidha alipiga marufuku kuwapiga faini wakinamama ambao wanajifungulia nyumbani.


Hata hivyo aliwahamasisha akina mama hao kujifungulia Hospitali ambapo ni salama kwa afya zao.


“Kutoza faini kwa mzazi aliyejifungulia nyumbani ni jambo ambalo limesitishwa, hivyo ninawatangazia rasmi kupitia mkutano huu kwamba tozo hizi zimesitishwa, hivyo mtu yoyote atakayeendelea kutoza mimi nitashughulika naye.” Alipiga marufuku Mkuu huyo wa Wilaya

Halikadhalika amewaomba wananchi hao kumpa ushirikiano.


“Ndugu zangu Wananchi! tukifanya kazi kwa ushirikiano tutapata maendeleo” Aliomba Mwenda.


Hayo yote yamekuja baada ya wananchi hao kuibua kero mbalimbali mbele ya Mkuu huyo wa Wilaya ambapo alizitatua papo hapo.


Akijibu kero za Wananchi Afisa Ustawi wa Jamii kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Happines Alex alisema kuwa tayari Serikali ilikwisha leta fedha za dawa, hivyo dawa zipo katika vituo vyote na Hospitali.


Kwa upande wake mmoja wa Wananchi aliewasilisha kero yake mbele ya Mkuu huyo wa Wilaya, Pelepetuwa Makala alimshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuja katika kata yao na kutatua kero zilizokuwa zikiwakabili hasa kwa upande wa afya na elimu.


“Napenda kumshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutuhakikishia kuwa kero ya upatikanaji wa dawa sasa imekwisha na katika upande wa Walimu kuhakikisha wanakaa katika vituo vyao vya kazi.”


Naye muinjilisti wa kanisa la KKKT Kisiriri, Daudi Napegwa alisema kuwa ujio wa Mkuu huyo wa Wilaya umeleta hamasa, faraja na matumani mapya  kwa wananchi kwa sababu kero ambazo walizokuwa nazo zimepata majibu stahiki toka kwa mkuu huyo wa Wilaya.


“Ninamshukuru sana mkuu wetu wa Wilaya kwa sababu ujio wake umefanya tuone suala la umeme, upatikanaji wa maji, walimu kukaa katika vituo vya kazi, upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na hospitali vimepata majibu stahiki.” Alisema Napegwa.

Mkuu wa Wilaya alifanya ziara kata ya kisiriri, Old Kiomboi, Kaselya, Ndulungu na akitarajiwa kufika katika kila kata zilizopo katika Wilaya hiyo.


Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amewataka Watumishi kuishi katika vituo vyao vya kazi. Picha na Hemedi Munga

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages