Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua madawati wakati alipotembelea Shule ya Msingi Chikoko wilayani Ruangwa Julai 23, 2021. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya (wa pili kulia) wakati alipokagua ujenzi wa maabara katika Shule ya Sekondari ya Makanjiro wilayani humo, Julai 23, 2021. (Picha na Ofisi a Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa madarsa katika Shule ya Msingi ya Chikoko wilayani Ruangwa, Julai 23, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chinokole wilayani Ruangwa, Julai 23, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
************************
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji vyote nchini vikiwemo na vya wilaya ya Ruangwa, Lindi.
Amesema suala la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali katika awamu hii, hivyo suala la upatikanaji wa huduma ya maji ni endelevu. “Tutaendelea kuboresha miradi ya maji ili maeneo yote nchini yapate maji ya uhakika.”
Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Julai 23, 2021) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji vya Mpara, Mtimbo, Mmawa, Chikoko, Chinokole na Kilimahewa wilayani Ruangwa.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha wananchi wote nchini wanapata huduma hiyo karibu na maeneo yao ya makazi. Amewataka waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu imedhamiria kuwatumikia.
Akizungumzia kuhusu tatizo la maji wilayani Ruangwa amesema Serikali inatekeleza ujenzi wa mradi wa maji wa Mbwinji ambao unatoa maji Ndanda hadi Ruangwa. “Mradi huu mkubwa unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la upatikanaji wa maji wilayani Ruangwa.”
Waziri Mkuu amesema mbali na huduma ya maji safi na salama, pia Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo nchini, hivyo amewataka wananchi wafanye maandalizi ya kufikisha nishati hiyo katika makazi yao.
Amesema Mheshimiwa Rais Samia anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme nchi nzima vikiwemo na vijiji vya wilaya ya Ruangwa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.
Pia Waziri Mkuu amesema wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zote zimeshabebwa na Serikali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇