Na. Georgina Misama - MAELEZO
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema katika siku 100 za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Sekta ya nishati imepeleka neema kwa wananchi wa maeneno mbalimbali huku akitaja kuwa takribani vijiji 400 vimefaidika na umeme kupitia mradi maalum wa REA.
Akizungumza hivi karibuni katika Kipindi Maalum cha Siku 100 za Rais Samia tangu aapishwe Machi 19, 2021 kilichorushwa na vituo mbalimbali vya televisheni nchini, Dkt. Kalemani amesema kwamba Vijiji 400 vimefikishiwa umeme ndani ya siku hizo na kufanya jumla ya vijiji 10,361 katika ya 12,268 kuwa na umeme nchini
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kutuwezesha kufanya kazi yetu kwa wakati, katika hizi siku 100 tumepeleka umeme vijiji 400 na tumepokea maelekezo yake kwamba ndani ya miezi 18 tuwe tumekamilisha vijiji vyote vilivyobaki. Na mimi nasema miezi 18 inatutosha hivyo tunatarajia ifikapo desemba, 2022 tutakuwa tumekamilisha kupeleka umeme kwa vijiji vyote vilivyosalia”, alisema Dkt. Kalemani.
Aidha, Dkt Kalemani aliongeza kwamba kwa mwaka huu wa fedha kiasi cha sh. trillion 1.24 kimetengwa kwa ajili ya kwenda kukamilisha zoezi la kusambaza umeme kwa vijiji vilivyobaki ambapo mpaka sasa Vijiji 10362 tayari vimefikishiwa huduma hiyo kati ya vijiji vyote 12268 vilivyopo hapa nchini. Zoezi hilo litakapokamilika Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kwa nchi za Afrika katika suala la kusambaza umeme vijijini.
Dkt. Kalemani pia alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuweka nguvu kubwa kwenye kuendeleza sekta ya nishati kwa ujumla wake ambapo mwaka huu wa fedha Wizara yake imepewa sh. trillion 2.385 fedha ambayo imeongezeka kwa asilimia 8 ukilinganisha na kiasi cha shilingi trillion 1.97 za mwaka wa fedha uliopita.
Akizungumzia vyanzo vya uzalishaji umeme nchini Dkt. Kalemani alisema kwamba vyanzo vikuu vya nishati ya umeme nchini ni gesi na maji ambapo hivi sasa asilimia 68 ya nishati hiyo inatokana na gesi na kiwango kilichobaki kinatokana na maji. Wakati huo huo alielezea mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wa Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) unaogharimu kiasi cha sh. bilioni 382 unaendelea kwa kasi kwani ndani ya miezi mitatu utekelezaji wake umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 52.
Miradi mingine ya kuzalisha nishati nchini ambayo tayari imetengewa fedha ni mradi wa mto Malagalasi ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 49 na kuwanufaisha wakazi wa Kigoma, lakini pia kuna mradi wa kusindika na kuchakata gesi (LNG) utakaogharimu Dola bilioni 30 ambapo wakazi wa Mkoa wa Lindi watanufaika na mradi huo kwa ajira zinazotarajiwa kufikia elfu 20.
Pindi miradi hiyo ya kuzalisha umeme itakapokamilika, uzalishaji wa umeme nchini utakuwa umefikia megawati 5000 ambapo kwa kiasi hicho Tanzania itakuwa imejitosheleza kwenye matumizi ya majumbani, viwandani pamoja na kuendeshea mradi wa treni ya kisasa ya SGR na pia itaweza kuuza umeme huo nchi jirajini. Dkt. Kalemani anatoa rai kwa Watanzania wote kuunganisha umeme majumbani mwao kwani gharama za huduma hiyo sasa zimeshushwa lakini pia kuchangamkia fursa za ajira pamoja na biashara zitakazotokana na kupatikana kwa umeme huo ili kujikomboa kiuchumi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇