Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania TEC katika ukumbi wa AMECEA Kurasini, Dar es Salaam leo 25 Juni, 2021.
Kurasini, Dar es Salaam, leo
Rais Samia Suluhu Hassan amesema, Taaisisi za Dini nchini ni muhimu kwa kuwa zina mchango mkubwa katika kudumisha amani, kustawisha maisha ya wananchi na kupambana na umasikini.
Rais Samia amesema hayo alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Makao Makuu ya Baraza hilo, Kurasini jijini Dar es Salaam, leo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu, imesema, Rais amewasihi Watanzania kuendelea kuvumiliana kwenye tofauti za Kidini zinapojitokeza ili kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini.
Rais Samia, amesema amani na utulivuni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya taifa hivyo vyema viongozi wa dini zote nchini kuendelea kuhubiri amani kwa waumini wao.
Pia Rais amewaomba Maaskofu na viongozi wengine wa Dini kuwakumbusha waumini wao kuhusu umuhimu wa kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona.
Rais Samia pia ametumia mkutano huo na Viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kueleza mipango ya Serikali ya miaka mitano kuwa ni pamoja na kudumisha mema yote ya Awamu zilizotangulia na kubuni mengine mapya.
Amesema Serikali imejipanga kuendeleza kukuza uchumi ili kupambana na umasikini na tatizo la ajira kwa kuboresha mazingira ya biashara.
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga amemuhaklikishia Rais Samia kuwa Baraza hilo litaendelea kushirikiana na Serikali anayoiongoza kwa lengo la kuwaletea Wananchi maendeleo.
Askofu Mkuu Nyaisonga amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kupokea majukumu ya Urais na kuongoza Taifa kwa utulivu na amani. Kuonyesha nia thabiti ya kushirikiana na ulimwengu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona.
Aidha, Askofu Mkuu Nyaisonga amemshukuru Rais Samia kwa kutenga muda na kuwasikiliza ambapo ameelezea hatua hiyo ni kuonesha nia ya dhati katika kukuza taifa lenye mshikamano, maridhiano, na maendeleo ya kweli.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇