LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 26, 2021

RAIS SAMIA AWATAKA WATANZANIA PAMOJA NA TAHADHARI WASIACHE KUMUOMBA MUNGU KATIKA MAPAMBANO NA CORONA

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi wa TEC, Jijini Dar es Salaam, jana.


Na Georgina Misama, TEC

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kila mmoja kwa dini yake wasiache kumuomba Mungu katika kupambana na ugonjwa wa corona sanjari na tahadhari ambazo zinachukuliwa katika kuepusha maambukizi ya ugonjwa huo.


Akihutubia katika mkutano wake na Viongozi Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), uliofanyikia Kurasini  Jijini Dar es Salaam, jana,  Rais Samia amesema hivi sasa Dunia inakabiliwa na ugonjwa wa Covid 19 wimbi la tatu na Tanzania ina wagonjwa waliopata maambukizi hayo hivyo amewaomba Maaskofu pamoja na viongozi wa dini mbalimbali kumlilia Mungu kwani yeye ni muweza wa yote.


“Nawaomba Maaskofu pamoja na viongozi wengine wote  wa dini nchini pamoja na njia zote za kisayansi tutakazozitumia tusisahau kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kutuepesha  na kutuhifadhi na maradhi haya kwani yeye ndie muweza wa yote.


Nimeangalia kwenye kitabu nilichonacho na nimeona kwenye Zaburi 91:4 kuna maneno ya Daudi, napenda kumnukuu, "Mungu atakufunika na mbawa zake na chini ya mbawa zake utapata hifhadhi, uaminifu wake kwa waja wake utakuwa ndio ngao na ngome  yetu utapata usalama kwake" na ndiyo maana nasisitiza tumuombe Mungu, atuwekee mkono, atufunike na mbawa zake”, alisema Rais Samia.


Rais Samia alifafanua kwamba  Dunia hivi sasa inapita katika wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona ambapo Tanzania ilipitia kwenye wimbi la kwanza na la pili  na sasahivi inakabiliwa na  wimbi la tatu  kwani ishara  za kuwepo kwa wagonjwa waliopata maambukizi hayo ndani ya nchi zinaonekana.


Pamoja na hayo,  Rais Samia ametambua msimamo dhabiti wa  Kanisa  Katoliki  katika kupambana na ugonjwa huo na kuwataka viongozi wa dini nchini kuwakumbusha waumini wao, umuhimu wa kujikinga na kuchukua tahadhari zote zinzoelekezwa na wataalam wa afya dhidi ya ugonjwa wa corona kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.


Kuhusu changamoto zilizowasilishwa na Rais wa Baraza la Maaskofu nchini ambazo zilijikita  katika kutoa huduma kwa jamii ikiwemo kodi kubwa, kodi za ardhi, umilikishwaji wa ardhi na makato ya ajira kucheleweshwa kwa ruzuku kutoka Serikalini, Rais Samia alisema amezipokeapokea na yupo tayari kukaa na wataalam wake ili kuyapatia ufumbuzi na kuimarisha huduma hizo zinazotolewa na Kanisa Katoliki.


Kiongozi wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu  Gervas Nyaisonga alisema Kanisa linaendelea kuwasaidia Watanzania kupambana na umasikini hasa katika kupata elimu bora pamoja na huduma bora za afya ambapo shule na hospitali za kanisa hilo zinahudumia Watanzania wote bila kubagua.


“Lengo la Shule zetu sio kufanyabiashara bali kutoa huduma bila kujali uwezo wa wazazi wanaotaka kuelimisha watoto wao kama ilivyo Sera ya Serikali yako ya Awamu ya Sita”, alisema Askofu Nyaisonga.


Kanisa katoliki nchini pamoja na huduma za kiroho pia linaendesha huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa hudima za afya na elimu ambapo hadi hivi sasa linamiliki shule za awali hadi sekondari zipatazo  754, hospitali pamoja na vituo vya afya takribani 464, ambapo asilimia 80 ya huduma hizo zimewekwa Vijijini sehemu ambazo uhitaji ni mkubwa zaidi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages