LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 19, 2021

RAIS ANAPOTARAJIA KUKUTANA NA NDOTO ZA MABILIONEA NYAMAGANA, AKAKUTANA NA WAGOMBEA MIRATHI!

Nyamagana, Mwanza

Rais Samia Suluhu Hassan kamaliza ziara yake mkoani Mwanza kwa kuzungumza na vijana wa taifa hili kupitia vijana wa mkoa wa Mwanza na Kanda ya ziwa kwa ujumla. Namshukuru Mungu kuna michuano ya soka huko Ulaya inaendelea ikatufanya tusahau yaliyojiri Nyamagana.


Tusidanganyane, tulichokiona Nyamagana ndiyo taswira ya vijana wa taifa hili walio wengi, wasomi kwa wasio soma tofauti kwenye ujenzi wako sawa. James Mbatia alipolalamikia mitaala ya elimu kipindi chote alipokuwa Bungeni alionekana hana maana! Katuumbua.


Rais Samia Suluhu Hassan alitoa fursa za vijana kuongea nae, waseme changamoto zao, nchi hii ni kubwa, nchi ina mambo mengi,  Rais si nabii wa kujua kwenye mifugo kuna shida gani, kwenye uvuvi kuna matatizo gani, kwenye madini kuna nini, Rais akataka kujua kwenye kilimo kipi kinawapa taabu vijana kuwa mabilionea kupitia kilimo.! Je ni mbegu za GMO? Uhaba wa masoko? Rais aliwaza mbali kuliko vijana wenyewe.


Kwanini vijana? Nguvu ya uchumi wa nchi iko kwa vijana! Kama kuna fursa za kiuchumi zinahitajika kulisukuma taifa mbele basi fursa hizo zinawalenga vijana. Mama akatenga penalti wapige, vijana si tu wamepaisha ila kwa uwakilishi ule penalti imepigwa ikawa mpira wa kurusha.


Tatizo ni nini? Vijana walio wengi maono yao ni namna gani wapate hela ya kula na kunywa. Hela hii haihitaji sana uwekezaji wa muda mrefu bali maono ya muda mfupi. Akili hizi zimewekezwa kwenye teuzi. Vijana wateuliwe u DC, U RC, u DAS. Aibu🙈


Rais alitegemea kukutana na hoja za vijana zinazoonesha namna gani vijana wapatiwe fursa za mitaji, misamaha ya kodi kwenye baadhi ya vitu kama matrekta ya kilimo, mikopo isiyo na masharti magumu kwenye taasisi za kifedha. 


Nyamagana Rais Samia alitegemea kukutana na hoja zenye kuonesha miaka hamsini ijayo taifa liwe la aina gani, mama akakutana na hoja za namna gani walioteuliwa wanaendelea kuaminiwa nae kwenye nafasi zao, na wale wasioteuliwa wanaingiaje kwenye nafasi za kuteuliwa mana wanajua kuna nafasi hizo😳🙈.


Ukisikiliza hoja za pale Nyamagana mbele ya Rais unaona kabisa Rais alikuja kusikiliza hoja za mabilionea watarajiwa ila ajabu akakutana na hoja za wagombea mirathi. Mama akafa moyo, kwenye hotuba akaanza kufafanua mpaka dhana nzima ya ujana! Ukimsikiliza Rais kwenye maana ya ujana utaona kuwa badala ya kuongea na vijana, alianza kutoa semina elekezi. Mwisho akakidhi matarajio yao ya muda mfupi, akawambia kuna mkeka wa wakuu wa wilaya unakuja. Wakashangilia.


Pale Kenya wiki hii wamempoteza bilionea Christopher Kirubi kwa saratani. Watanzania tarehe 15 June 2021 tumepoteza mabilionea Nyamagana kwa uwezo wa kufikiri. Christopher Kirubi alitaka kuwa bilionea akawekeza kwa kutumia fursa za nchini kwake, vijana wa Watanzania wanataka kuitwa mheshimiwa mkuu wa wilaya wamewekeza kwenye kujipendekeza.


Angalia jumuia za vyama vya siasa za makundi ya vijana. Hazina maono. Wakipata fursa ya kuongelea jambo mwisho wa hotuba lazima uulize ana elimu gani huyu mtu*. Ukiambiwa elimu yake bado unahoji alipataje hii nafasi.


Nchi nzima inakusikiliza unapewa kisemeo unaanza kusema Mheshimiwa Rais sisi vijana tunakuunga mkono. Baada ya kumuunga mkono kinafuata nini? Aliyekuuliza nani? Mama kasema anawateua kutegemea na bidii yenu ya kusifu na uimbaji pambio?


Kundi hili la vijana ndilo lenye watu wasomi, lakini, nasema tena lakini, ikitokea mheshimiwa Rais akakutana na kundi la Mama Ntilie,  ndiyo utaona tofauti ya elimu maisha na elimu teuzi.

Vijana waliohudhuri, wakiwa kwenye Mkutano wao na Rais Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.


#Imeandikwa na Diwani wa Kata ya Kongolo- Magu na Mwanafalsafa Ndugu Herbet Faustine

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages