Na Mwandishi Maalum
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umewaalika wanachama wake na wananchi kwa ujumla kutembeela banda la Mfuko huo ili kupata taarifa za huduma mbalimbali zikiwemo zile la kumiliki nyumba kwa gharama nafuu.
Akizungumza kwenye banda namba 13 la Mfuko huo kwenye viwanja vya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, Juni 29, 2021 Meneja Uhusiano wa Mfuko huo Bw. James Mlowe alisema, Mfuko umedhamiria kwa dhati kuhakikisha unawawezesha wanachama wake na wananchi kwa ujumla kumiliki nyumba na viwanja sehemu mbalimbali nchini kwa kulipa kidogokidogo.
“Tumeingia makubaliano na benki ya Azania ambayo itawawezesha wanachama na wananchi kukopa mikopo ya makazi (Mortgage loan) kwa masharti nafuu ili kununua nyumba na viwanja vinavyomilikiwa na PSSSF kupitia uwekezaji iliyoweka sehemu mbalimbali nchini kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Shinyanga, Tabora, Mtwara na Iringa na mradi wa viwanja vya gharama nafuu viko katika mikoa ya Ruvuma, Kagera, Tabora, Iringa, Katavi, Morogoro, Dar es Salaam, Rukwa, Lindi na Mtwara.
Akifafanua zaidi kuhusu masharti ya kukopa nyumba na viwanja Meneja huyo alisema, mteja atalazimika kuweka rehani ya asilimia 10% ya thamani ya mkopo au mali ya thamani hiyo kwa dhamana ya mkopo na kiwango cha juu kabisa ambacho mteja anaweza kukopeshwa na benki ni asilimia 90% ya thamani yote ya nyumba au kiwanja.
“Mteja atakapokamilisha malipo yake atakabidhiwa hati yake ya nyumba au kiwanja na benki ya Azania na muda wa marejesho ya mkopo ni kipindi kisichozidi miaka 15 kwa mkopo wa nyumba na miaka miwili kwa mkopo wa kiwanja.” Alifafanua Bw. Mlowe.
Kuhusu huduma nyingine ambazo wananchi na wanachama watafaidika kwa kutembelea banda hilo ni pamoja na Wanachama kupata taarifa za michango, uwekezaji, mafao ya uzazi, pensheni ya uzeeni, Pensheni ya Warithi, Pensheni na Ulemavu.
Maonesho hayo ya siku 13 yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu” yameanza Juni 28 na yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan Julai 5, 2021.
Afisa Uhusiano Mkuu Mfuko wa PSSSF, Bi.Fatma Elhady (katikati) akimuhudumia mwanachama. Kulia ni Afisa wa fedha Mariam Mbarouk
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇