LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 26, 2021

KATIBU MKUU WA CCM AWATAKA UWT KUPAMBANIA VILIVYO UPATIKANAJI WA MIKOPO YA 4% KWA WANAWAKE KUTOKA HALMASHAURI

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewataka Viongozi wa Jumuiya hiyo hasa Wabunge wa Viti Maalum, kusimama kidete katika kusimamia upatikanaji wa 4% ya mikopo kwa Wanawake kutoka katika Halmashauri.


Chongolo amesema upatikanaji wa mikopo hiyo utawawezesha Wanawake kujihakikishia upatikanaji wa Mitaji ya kuwakwamua Kiuchumi na kuwaomba pia Viongozi wa UWT kulifanya suala la mikopo hiyo ya 4% kwa Wanawake kutoka iwe ni Ajenda ya Kudumu.


“ Niwaombe Wabunge wa Viti Maalumu kwa kuwa wanaingia kwenye Mabaraza ya  Halmashauri wakasimamie upatikanaji na usimamizi wa hizi fedha na waandae taarifa kwa ajili ya upatikanaji wa fedha hizo”, amesema Chongolo.


Amesema hayo wakati akizungumza kwenye Kikao cha kawaida cha Baraza Kuu la Taifa la UWT katika Ukumbi ndani ya Jeno la White House, Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma, leo.


Chongolo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye kikao hicho alisema, miongoni mwa madhumuni 10 yaliyoko kwenye Katiba ya UWT yanayoakisi madhumuni ya kuanzishwa kwa Jumuiya Hiyo ni kutetea maslahi ya Wanachama wa Jumuiya hiyo na Wanawake wote kwa jumla.


Kutokana na dhumuni hilo Chongolo aliwataka Wajumbe hao wa Baraza pamoja na waaalikwa wakatekeleze jukumu hilo ili waweze kuwasaidia wanawake wa Tanzania.


Chongolo pia alisisitiza Viongozi wa UWT wa Ngazi Mbalimbali kubadili mfumo wa vikao vyao na kuwataka wakajikite katika kujadili mambo yenye kuongeza msukumo wa kuleta maendeleo katika jamii kwa kujadili kwa kina changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake wa Tanzania.


“Kwa kwa UWT vikao vyake huanzia ngazi ya Tawi basi ni vema mketi na kujadili Changamoto za wanawake katika Matawi yetu”, alisema Chongolo.


Ametaka Baraza hilo liwe linajua fedha kiasi gani nchi nzima zimetengwa, zimetolewa kwa kina mama wangapi kwani anazotaarifa  kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakijinufaisha na fedha hizo.


Chongolo amesema matarajio ya chama ni kuona viongozi wanakuwa na agenda zenye mashiko katika jamii huku akihoji ni kwanini Baraza la mwaka huu halina agenda ya matumizi ya fedha asilimia 4 zinazotolewa katika Halmashauri.


“Kuanzia sasa agenda ya kudumu ya Baraza kuu la Jumuiya  iwe matumizi ya fedha asilimia 4 za wanawake zinazotolewa katika halmashauri.


Tujue nchi nzima fedha kiasi gani zimetengwa, zimetolewa kwa  kina mama wangapi na kina mama wangapi  wamenufaika sababu kina mama wengine ndio kina sie wengine wanatengeneza miradi ya kuwanufaisha ninyi,sisi kama chama hatupo tayari hili litokee,” amesema.


Amesema Baraza hilo ndio 'furum' ya kuwazungumzia wanawake kuhusiana na fedha hizo ambapo amedai Halmashauri ya Kinondoni pekee imetenga sh. bilioni 4 ambapo amehoji ni kwanini mwanamke alalamike suala la mtaji.


“Kwa sababu hii ndio forum ya kutengeneza mfumo sahihi msiwaache kina mama wenzetu mimi nimetoka Kinondoni mwaka huu wametenga bilioni 4 kwanini wanawake walalamike changamoto ya mitaji,”amesema.


Chongolo ameitaka UWT  kutumia vikao kuwasaidia wanawake na sio kuvitumia kusengenyana na mambo  yao binafsi.


Amesema kwa sasa ukiona idadi ya wajumbe kwenye vikao imekamilika ujue kuna mtu anataka kushughulikiwa ambapo amedai jambo hilo sio zuri.


“Uhai wa chama ni vikao ni muhimu kwani ndio sehemu ya kujadili mambo yetu na uzoefu unaonesha vikao vyetu vingi vinakosa tija.Nasema kwa sababu tumekuwa na vikao kuanzia kamati ya utekelezaji,baraza kuu na vikao vingine  vya juu muda mwingi sana katika vikao hivi ukiona ‘Colum’ imetimia  na wajumbe wamefika ujue kuna mtu wanataka kumshughulikia.


“Vikao hivi vinafanyika ndani ya Jumuiya katika chama ambacho kimepewa nafasi ya kuongoza Nchi na kazi ya kuongoza Nchi sio kazi ya lelemama alisema Mwalimu Nyerere (Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na sisi ndio tunatoa kazi ya uongozi sisi ni lazima tuwe mwarobaini wa kule tunapotoka.


“Kuna kina mama kila eneo sasa wanatakiwa wakuone wewe kama daraja vikao ndio vinatakiwa kuwa sehemu mahasusi sisi tumebahatika kuwemo katika vikao.


Sisi tunawajibu wa kuheshimu msihangaike na mambo ya watu hangaikeni na mambo ya maendeleo UWT isiwe kwenda kujadili huyu mrefu ama mfupi jadilini mambo ya maendeleo tuwe ni viongozi ambao tunajitengenezea daraja uongozi usiwe ni kujadili sisi kwa sisi tujadili inshu,” amesema.


Chongolo amesema yeye ni mgeni machoni mwa watu lakini anauzoefu wa zaidi ya miaka 20 na ameingia katika vikao muhimu vya chama hicho ambapo amedai yeye atasimamia taratibu ili kujenga maadili ndani ya chama.


“Niwaambie ninavyoongea nacheka hivi lakini mimi ni bingwa wa kusimamia taratibu ni lazima tujenge maadili kwenye chama chetu na lazima tusimamie hili na tuheshimu kwa dhati.


“Mimi ni Katibu Mkuu mpya ila mwenye kwao wanamjua niseme kweli mimi ni mgeni machoni mwa wengi lakini huu ukumbi nimeingia zaidi ya miaka 20 na nimebahatika kweli kuwa kijana mdogo ambaye nimeingia   katika vikao muhimu vya Sekretarieti,Kamati Kuu,Maadili Taifa wakati ule nilikuwa Afsa lakini nimekuja kuwa Mkuu wa Maafsa,” amesema.


Chongolotibu amesema wanawake ni jeshi kubwa lakini limekuwa likionekana wakati wa uchaguzi tu hivyo amelitaka kujitokeza wakati wote kukipambania chama.


“Wanawake ni Jeshi kubwa lakini halionekani katika shughuli za kawaida ninyi mmekuwa Jeshi kubwa wakati wa uchaguzi tu jambo hili sio sawa Jeshi  kubwa ni lile linalofanya kazi kubwa wakati wa Amani na kuongoza mapambano.


“Na sisi wakati wa kawaida ndio wakati wa kuimarika na kuhamasisha na kuusimamia na uhai ili wakati wa pambano Jeshi letu litusaidie.Mwakani kuanzia  Februari  tunaanza uchaguzi na hicho ndio kipimo cha kuona kwamba ninyi ni jeshi kubwa na maana nyingine,” amesema.


Amesema licha ya wanawake kuwa ni jeshi kubwa lakini baadhi wamekuwa wakifanya matendo ambayo sio mazuri.


“Wanawake ni Jeshi kubwa lakini baadhi yenu wanawaangusha Jeshi hili hasa kwa vitendo vyao na matendo yao na hivi karibuni tumeona mambo ya aibu yanafanyika ni maeneo mengi hayatujengei sura nzuri yanachafua sura yetu.


“Nikuhakikishie sisi ni wakali na tutaendelea kuwa wakali mtu yeyote akifikia kwamba anauwezo wa kufanya mambo yake ya hovyo na sisi tukamchekea na kumwangalia sio wakati huu.Ukiwa kiongozi lazima uwe unajiheshimu na unajua majukumu yako,”amesema.


Chongolo pia amesema wale wanaojipanga na kujipitisha kugombea nafasi mbalimbali wanatakiwa kuachwa kwani hakuna mahali panaporuhusu utaratibu huo mbovu.


“Mimi niwaombe mkisikia dalili watu wanaojipanga katika nafasi muwaache hata UWT hakuna mahali panaporuhusu utaratibu huu na utaratibu huu ni wa hovyo na hautusaidii kupata viongozi wazuri.


“Nimeona niliseme hilo kwa sababu moja ya sifa ya vikao vyetu mara nyingi hutumikia kupanga safu na hutumika kutengeneza makundi badala ya kutengeneza umoja hutumika kutengeneza miundombinu ya kujiwekaweka mahali fulani ili ukubalike badala ya kutengeneza miundombinu ya chama chetu kiheshimike,” amesema.


Amesema ndani ya chama wamefanya mapitio na kugundua wameteleza kwenye kusimamia misingi kuanzia ngazi ya shina na wameanza kwenda katika mashina kuwahamasisha wananchi kwani ndiko wanakopatikana.


Chongolo aliendelea kuwapongeza wanawake waliochaguliwa katika Serikali na kuwataka kuendelea kuwa Waaminifu, Waadilifu na Wachapa Kazi ili kukikidhi matarajio ya wananchi na aliyewateua.


Baraza hilo chini ya Mwenyekiti wa UWT Gaudentia Kabaka kiliazimia kuendelea kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan Rais na wamehidi kuendelea 'kukoleza rangi ya maendeleo katika Taifa.


Kikao hicho kilianza kwa mwana mama mahiri, Katibu Mkuu wa UWT Queen Mlozi kutoa maneno ya utangulizi, ambapo aliwataka Wajumbe kumsikiliza Katibu Mkuu Chongolo ili baada ya kikao wakayafanyie kazi maelekezo atakayotoa kwenye hotuba yake.

Katibu Mkuu wa UWT Queen Mlozi akimkabidhi zawadi maalum Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo kama ishara ya UWT kutambua mchango wake katika Chama, Wakati ya Mkutano wa Baraza Kuu la UWT mjini Dodoma, leo.

Katibu Mkuu wa UWT Queen Mlozi akitoa utangulizi mwanzoni mwa Kikao hicho ambapo pia alimkaribisha Mwenyekiti wa UWT Gaudentia Kabaka kutoa maneno ya ufunguzi wa Kikao hicho na kumkaribisha Katibu Mkuu wa CCM kuongea.
Mwenyekiti wa UWT Gaudentia Kabaka akitoa maneno ya ufunguzi wa Kikao hicho na kumkaribisha Katibu Mkuu wa CCM kuongea.

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo akizungumza kwenye kikao hicho.
Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo akizungumza kwenye kikao hicho, huku viongozi na wajumbe wa kikao hicho wakimsikiliza.

Wajumbe mbalimbali wakiendelea kumsikiliza Chongolo ukumbini kwenye kikao hicho👇







+++
Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa UWT baada ya kuhutubia kikao hicho.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages