Dar es Salaam, Tanzania.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa daraja jipya la Tanzanite (New Selander Bridge) jijini Dar es Salaam kufuatia ujenzi kufikia asilimia 83.5.
Waziri Mkuu ameelezea kuridhishwa kwake, alipotembelea ujenzi wa mradi huo na kukagua maeneo mbalimbali, jana.
Mradi wa ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilomita 1.03 na upana wa mita 20.5 ambalo ujenzi wake unagharimu jumla ya Sh. Bilioni 243.75, unatarajiwa kukamilika Desemba 14, mwaka huu.
Majaliwa amesema Watanzania wanaofanyakazi katika mradi huo wahakikishe wanafanyakazi kwa umakini ili mradi utakapokamilika waweze kuwa na uwezo wa kujenga wenyewe daraja kama hilo.
“Tuhakikishe kila mmoja anakuwa mahiri katika fani yake kama ni kuchanganya zege au kusuka nondo, ili kila mmoja awe na uwezo wa kujenga daraja lingine kama hili.", amesema Majaliwa.
Mapema, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale alisema mradi wa ujenzi wa daraja hilo kwa sasa upo katika hatua za ukamilishwaji wa eneo la juu na tayari mkandarasi ameshalipwa Sh. Bilioni 175.4.
Wazairi Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua ujenzi wa Daraja hilo, jana.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇