Kikao kikiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe Maalum wa Rais wa Shirikisho Urusi kuhusu masuala ya Afrika na Mashariki ya Kati Mhe. Mikhail Bogdanov katika Ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe Maalum wa Rais wa Shirikisho Urusi kuhusu masuala ya Afrika na Mashariki ya Kati Mhe. Mikhail Bogdanov akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe Maalum wa Rais wa Shirikisho Urusi kuhusu masuala ya Afrika na Mashariki ya Kati Mhe. Mikhail Bogdanov pamoja na ujumbe wake katika Ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.
************************
Na Mwandishi wetu, Dar
Shirikisho la Urusi limesema
linaunga mkono jitihada zinazofanywa na Umoja wa Afrika katika kutatua
changamoto zinazolikabili bara hilo kwa kuwa matatizo ya Afrika
yanahitaji kutatuliwa na Waafrika wenyewe bila kuingiliwa na Mataifa
mengine.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe Maalum wa Rais wa
Shirikisho Urusi kuhusu masuala ya Afrika na Mashariki ya Kati Mhe.
Mikhail Bogdanov ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokutana na
kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) na kupongeza jitihada
zinazofanywa na Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kutatua changamoto
za kiusalama katika eneo la maziwa makuu.
Tunaunga mkono jitihada zinazofanywa na Umoja wa Afrika katika kutatua changamoto zinazolikabili Afrika kwa kuwa matatizo ya Afrika yanahitaji kutatuliwa na Waafrika wenyewe, amesema Bogdanov. Pia Naibu waziri huyo amepongeza jitihada zinazofanywa na Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kutatua changamoto za kiusalama katika eneo la maziwa makuu.
Aidha, Bogdanov ameongeza kuwa Urusi ni moja kati ya nchi
zinazoamini kuwa Afrika inaweza kutatua matatizo yake bila ya
kuingiliwa kutokana na mazingira yaliyopo na kwamba nchi hiyo ipo tayari
kushirikiana na Afrika hususani Tanzania katika kuleta amani na usalama
sambamba na kuchochea jitihada za maendeleo ikiwemo biashara na
uwekezaji.
Kwa upande wake waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amemuomba Waziri huyo
kuimarisha zaidi mahusiano ya diplomasia ya Uchumi hususani katika sekta
ya biashara na uwekezaji kutokana na takwimu zilizopo kuonesha kiwango
kidogo cha mahusiano ya kibiashara na uwekezaji.
Tumejadili masuala la
kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Urusi hasa katika sekta ya biashara
na uwekezaji, ambapo Mhe. Bogdanov ameahidi kulifanyia kazi suala hilo
na kuhakikisha kuwa tunakuza biashara na uwekezaji, amesema Balozi
Mulamula
Pia Balozi Mulamula amesema Tanzania iko tayari kuwa
mwenyeji wa mkutano wa ushirikiano kati ya Urusi na Afrika ambao
umepangwa kufanyika Afrika ambapo Umoja wa Afrika unajukumu la
kupendekeza nchi moja ambayo itakuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Amemuomba pia Naibu Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa
Shirikisho la Urusi kuhamasisha watalii kutoka Urusi kuja kwa wingi hapa
nchini na kwamba licha ya ugonjwa wa COVID 19 Tanzania imechukua
tahadhari zote zinazosisitizwa na Shirika la Afya Duniani
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇