LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 12, 2021

MPINA AIBUA BUNGENI HOJA NZITO YA WIZI WA DAWA ATAKA WABUNGE WASIPITISHE BAJETI KUMALIZA KWANZA TATIZO HILO NCHINI

 

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina akichangia bajeti ya Wizara ya Afya bungeni jijini Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina amewataka wabunge kutopitisha Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hadi suala la wizi wa dawa litakapotafutiwa ufumbuzi kwani limeleta
madhara na malalamiko  makubwa kwa wananachi kukosa dawa kwenye vituo vya Serikali vya  kutolea huduma.

Akichangia hotuba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2021/2022, Mpina amesema katika hotuba ya Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima imetaja kuwepo  tatizo la wizi wa dawa lakini Serikali haijaonesha ni kwa namna gani tatizo hilo lilivyo kubwa na hatua zilizochukuliwa kwa wezi hao wa dawa za wananchi.

“Mh. Naibu Spika nimesoma hotuba ya Waziri kuhusu suala hili nadhani iko ukurasa wa 61 lakini Mh Naibu Spika suala hili la wizi wa dawa linavyoripotiwa ni kubwa sana lakini nimeona kwenye hotuba ya waziri pale ni kama imeandikwa kama para moja hivi nataka niseme hivi kwa ufupi kwamba tatizo hili ni kubwa” amesema Mpina.

Mpina amesema Waziri wa Afya aliwahi kutangaza vita dhidi ya wezi wa dawa lakini dawa zimeibiwa Songwe ambapo alitangaza Waziri mwenyewe kuwa dawa zenye thamani ya milioni 13.5 ziliibiwa lakini pia Ukerewe dawa za milioni 200 ziliibiwa na kwenye taarifa yake anakiri kwamba wizi huo
unasababisha huduma za dawa zisiwafikie wananchi.

“Sasa hivi kweli leo hii Serikali imeshindwa kabisa kudhibiti hawa wezi wa dawa? Mpaka leo wanaendelea kuiba dawa? Nani anayeiba dawa hizi? anafanikiwaje kuiba dawa katika Serikali ambayo imejipanga kuanzia kwenye kitongoji, kwenye kijiji, kwenye kata , kwenye tarafa, kwenye wilaya, na ina vyombo vya dola kila sehemu hawa wezi wa dawa ni akina nani ambao hawawezi kukamatwa na kuadhibiwa” anasema Mpina

Mpina amesema kwenye taarifa ya Waziri angetuambia amekamata wezi wangapi toka ainze vita dhidi ya wezi wa dawa lakini hakuna, Nani ameiba dawa?
anafanikiwaje kuiba dawa na dawa hizi zinaibiwa zinakwenda kuuzwa wapi? nani ananunua dawa hizi, mtandao wa wizi huo nani anaufadhili mpaka kiasi kwamba tushindwe kukomesha suala hili.

“Sasa watu wanaiba dawa leo tunaenda kuidhinisha bajeti ya dawa zikaibiwe ni shida sana kupitisha bajeti ya waziri huyu ambaye yeye mwenyewe anakiri kwamba kutokana na wizi huu dawa haziwafikii wagonjwa sasa kama dawa haziwafikii wagonjwa Bunge hili lijishirikishe kikamilifu kuhakikisha kwamba kwanza tunamaliza tatizo la wizi wa dawa halafu ndio tupitishe bajeti” Mpina.

Mpina amesema bila kumaliza tatizo hilo la wizi wa dawa itakuwa ni tunawaongopea watanzania kuhusu suala hili la wizi wa dawa.

“Mh. Naibu Spika ukisoma kiambatisho cha sita ambacho Waziri amekisema yeye mwenyewe ukisoma yale matukio ukiukwaji mkubwa wa manunuzi watu wananunua dawa wanavyotaka wenyewe, watu wameiba dawa, watu wamefanya kila aina ya hujuma hatua kwa nini hazichukuliwi? Kwanini hatuambiwi “ alihoji Mpina

Mpina amesema ilitakiwa Serikali ije na mkakati mahususi wa kumaliza tatizo la wizi wa dawa kwa kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya dawa.

“Tulitegemea wezi wa dawa hawa tungekutana nao kila siku wana pingu mkononi kila kunapokucha, Serikali hii haiwezi kushindwa kudhibiti wezi wa dawa, tumeweza ufisadi, tumeweza uvuvi haramu, tumeweza hayo, tumeweza madawa ya kulevya leo hii tunakuja kushindwaje suala la wizi wa dawa kuna mtu hapa hajawajibika sawa sawa Mh Naibu Spika” amesema Mpina

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages