***********************
Na Mwandiahi Wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesema Wizara rasmi
inaanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa ambao utapitishwa
kupitia Bajeti ya mwaka ujao wa Fedha wa 2021/2022.
Mfuko huo utakuwa maalum kwa
ajili ya kusaidia wasanii kupata mitaji ambayo itawasaidia kufanya kazi
zao za Sanaa kwa ufanisi na tija kwa taifa pamoja na kuwapatia mafunzo
ya kuwaongezea uwezo wao wa kiutendaji.
“Bajeti ya Serikali kwa mara ya
kwanza inakwenda kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko huo ambao utakuwa
mkombozi mkubwa kwa wasanii wetu, kwani wataweza kupata mitaji kwa ajili
ya kufanya kazi zao za Sanaa na Kupata mafunzo ya kuongezeana uwezo”
amesema Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi amesema hayo wakati
wa Iftari maalum ya wadau wa Habari na DSTV iliyoandaliwa na kampuni ya
Multichoice Tanzania na kupewa jina la Media Showcase iliyofanyika Mei
6, 2021 Jijini Dodoma alipomuwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa.
Ameongeza kuwa Kampuni ya
Multichoice Tanzania imefanya kazi kubwa sana na Wizara ya Habari
inawashukuru kwa mchango wao ikizingatiwa ni wadau muhimu wa kimkakati
kwa maendeleo endelevu ya nchi.
‘’Nawapongeza Multichoice
Tanzania kwa uwekezaji mkubwa mlioufanya kwenye sekta ya Habari, nyinyi
ndio baba wa teknolojia ya Televisheni nchini, kwenye eneo hili mmekuwa
viongozi wazuri, mmeonesha njia kwa wengine, nawapongeza kwa kuanzisha
filamu zenye maudhui ya kitanzania na zinafuatiliwa sana’’ aliongeza
Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi amesema Serikali
itaendelea kuwaunga mkono na kuwaombea muendelee kuwekeza kwenye sekta
za Wizara na kuwaahidi kuzitatua changamoto wanazopitia ikiwezekana
kuzimaliza kabisa ili waendelee kufanya kazi zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Bodi ya Multichoice Tanzania Balozi Ami Mpungwe wakati akimkaribisha
Mgeni rasmi Dkt. Abbasi amesema Kampuni ya Multichoice imeajiri vijana
wengi Tanzania na imekuwa chanzo kizuri cha kukuza sekta ya Sanaa hapa
nchini na amewaomba wadau wa Sekta ya Sanaa kuendelea kushirikiana na
Multichoice ili kukuza Sanaa nchini na kuleta maendeleo.
Ameongeza kuwa vijana wengi
wamekuwa wakijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Filamu cha Akademia ya Filamu
ya MultiChoice cha nchini Kenya hatua inayowasaidia kuwaongezea ujunzi
ambapo wengi wamepata ajira na wamepata nafasi ya kushirikiana na
waongoza filamu wakubwa kutoka nje ya Tanzania.
Shughuli hiyo Iftari maalum pia
imehudhuriwa na baadhi ya Wabunge pamoja na wasanii mbalimbali wa filamu
kutoka Multichoice Tanzania wanaoigiza filamu za Jua Kali, Huba na
Pazia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇