LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 19, 2021

WAZIRI MKUU ATEMBELEA KIWANDA CHA MAGARI CHA GFA, ASEMA SERIKALI ITAENDELEA KUWAPA USHIRIKIANO WAWEKEZAJI

Na Said Khamis, Kibaha

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda kuunganisha magari cha GFA kilichoko Kibaha mkoani Pwani na ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wawekezaji wote kwamba Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano.


”Nimeridhishwa na kufarijika kuona hali ya kazi inayofanyika kiwandani hapa, niwahakikishie kwamba Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika uwekezaji wenu. Mheshimiwa Rais aliona kazi yenu kupitia mitandao na akanituma nije nione”.


Waziri Mkuu ambaye ametembelea kiwanda hicho leo (Jumatatu, Aprili 19, 2021),amesema hayo ndiyo mawazo ya viongozi wa nchi tangu Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufu na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.


”Mmewekeza kwa wakati sahihi na kwenye nchi sahihi na uwekezaji huu lazima utawaletea faida kwa sababu sera zetu za uwekezaji ni sahihi. Niwahakikishie kwamba Serikali yetu imejipanga vizuri katika kuwahudumia wawekezaji”.


Pia, Waziri Mkuu ameupongeza uongozi wa mkoa wa Pwani kwa kutumia vizuri fursa ya maendeleo ya viwanda nchini kwa kutenga ardhi ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji katika Halmashauri zake zote.


Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka Watanzania waendelee kuiunga mkono na kuiamini Serikali yao. Pia, Waziri Mkuu amewataka Watanzania walioajiriwa na kampuni hiyo wafanye kazi kwa bidii na wawe waaminifu na waadilifu.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amesema mkoa huo katika kipindi cha kuanzia 2015 hadi 2021 umejenga viwanda 1,100 na kufanya mkoa huo kuwa na viwanda 1,438 kati yake vikubwa ni 82 kikiwemo na cha GFA. “Viwanda hivi vimetoa ajira za moja kwa moja 50,000 na za muda 100,000”


Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa GFA, Bw. Jawaad Karmali alisema kiwanda chao kina uwezo wa kuunganisha magari ya aina yote kutokana na teknolojia waliyo nayo ila kwa sasa wameanza kwa kuunganisha malori.


Awali Mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo ameeleza kuwa mkoa huo ni wa Viwanda ambapo hadi sasa una vipatavyo 1438 kati yake vikubwa kama hicho cha magari alichotembelea ni zaidi ya 82.


Kwa upande wa Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Ali Jawad Karmali amesema GFA Wanajivunia kuwekeza nchini Tanzania na kuwa kiwanda cha kwanza kutengeneza magari nchini.


Karmali ameiomba serikali kuzielekeza Tasisisi zake ikiwemo Majeshi zisiwe zinaagiza magari kamili badala yake ziwe zinaagiza vipuri na baada ya kuviingiza nchini ziwe zinaipa GFA kazi ya kuunganisha vipuri hivyo na kuwa gari kamili lenye ubora kamili.


Vile vile alisisitiza kuwa anaamini changamoto ndogo ndogo wanazokutana nazo zitatatuliwa kwa kushirikiana na serikali ili kampuni hiyo iweze kushiriki kikamilifu kutimiza kaulimbiu ya Tanzania ya Viwanda.


Alisema kiwanda chao kimeajiri watumishi takribani 100, huku uwekezaji wao ukigharimu sh. bilioni 12. Uwekezaji huo unafanyika kwa awamu mbili, ambapo katika awamu ya kwanza wameshatumia sh. bilioni nne.

******

Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa akisiliza maelekezo kutoka kwa Baraka Samson, wakati alipofanya ziara ya kutembelea Kiwanda cha kutengeneza Magari GFA-Vehicle Assembling kilichopo Kibaha mkoani  Pwani ldo. Wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Ally Jawad Karmali.

Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa akisiliza maelekezo kutoka kwa, Elizabert Mwaya wakati alipofanya ziara ya kutembelea Kiwanda cha kutengeneza Magari GFA-Vehicle Assembling kilichopo Kibaha mkoani  Pwani leo. Kulia ni Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Ally Jawad Karmali.

Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi wa Kiwanda cha kutengeneza magari cha GFA-Vehicle Assembling kilichopo Kibaha mkoa wa Pwani, wakati wa ziara ya kukagua kiwanda hicho leo. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo. (Picha zote na Said Khamis)

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages