Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Wototo, Dkt. Godwin Mollel wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Himofilia ambayo hufanyika Aprili 17 kila mwaka lengo ikiwa ni kuwaleta pamoja watu wenye matatizo ya Himofilia duniani.
Dkt. Mollel amesema wananchi wakipatiwa elimu ya ugonjwa huo itawasaidia kupunguza madhara na vifo vitokanavyo na magonjwa yasioambukiza ikiwemo Himofilia na Selimundu.
Naibu Waziri alimuagiza Mratibu wa Mradi wa ‘Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma kwa Watu Wenye Magonjwa ya Damu,’ kwenda katika hospitali za rufaa, kanda na wilaya ili kutoa elimu ya ugonjwa huo ambayo itawasaidia watu wenye Himofilia kufika hospitali mapema.
“Dkt. Stella hakikisha unakwenda katika hospitali za kanda kutoa elimu hii, nafikiri itakuwa njia rahisi kuwafikia wataalamu wengi wa afya nchini,” amesema Dkt. Mollel
Amesema maisha ya watu wenye tatizo la Himofilia yanahitaji uangalizi mkubwa ili kuzuia uvujaji damu, ulemavu na vifo, hivyo hulazimika kupimwa ili kubaini aina ya Himofilia inayo msumbua mgonjwa na kupata matibabu ya kuchomwa factor (chembechembe za protini zilizokosekana mwilini) ili kusaidia kugandisha damu.
“Kama tunavyofahamu, Himofilia ni ugonjwa wa damu kukosa uwezo wa kuganda ambao unasababishwa na ukosefu wa kiwango cha kutosha cha chembechembe za protini zinazotakiwa kugandisha damu, hivyo husababisha damu kuvuja muda mrefu baada ya mgonjwa kupata jeraha na kuhatarisha maisha,’’ amesema Dkt. Mollel.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Mollel alishiriki kwenye maandamo ya kuadhimisha siku ya ugonjwa wa Himofilia duniani na alizindua dawa mpya ya Emicizumab ambapo Waziri alishuhudia mmoja wa wagonjwa wenye Himofilia akichomwa sindano Emicizumab.
Pia, Waziri alizindua gari la mradi wa ‘Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma kwa Watu wenye Magonjwa ya Damu.’
Naye Mkurugezi Mtendaji wa Hospitalli ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema mwaka jana Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi 10 barani Afrika zilizochaguliwa kupewa msaada wa dawa mpya ya Emicizumab kwa ajili ya wagonjwa wa Himofilia
“Mhe. Waziri, ninafurahi kukwambia kuwa Tanzania tumekuwa nchi ya nne barani Afrika kupokea msaada wa dawa hizi na kuanza kuitumia rasmi ambapo kwa Afrika Mashariki, Tanzania inakuwa nchi ya pili baada ya Kenya na nyingine zilizopokea dawa hizi barani Afrika ni pamoja na Zambia na Cameroon”.
“Dawa hizi ni ghali sana hivyo kwa kuwa mradi huu ni wa miaka mitatu tunaomba Serikali ione namna ambavyo itaendeleza huduma hii iweze kuwa endelevu baada ya mradi kuisha muda wake,” amesema Prof. Museru.
Mmoja wa wanachama wa chama cha watu wenye magonjwa ya Himofilia, Bi. Regina Shirima aliitaka jamii hasa kinababa kushirikiana na kinamama katika kuwapeleka hospitali watoto wenye himofilia kwani baadhi ya kina baba wamekuwa wakiwakimbia wake zao baada ya kubaini mmoja ya watoto ana tatizo la Himofilia.
“Tunawashukuru wataalamu wa MNH akiwamo Dkt. Stella, tunawapigia simu usiku mara mtoto anapovuja damu,” amesema Bi. Shirima.
Hospitali ya Taifa Muhimbili ikishirikiana na wadau wa afya Novo Nordisk Foundation (NNF) na Novo Nordisk Hemophilia Foundation (NNHF), ilianzisha mradi huu ili kuongeza kasi ya upatikanaji huduma kwa watu wenye magonjwa ya damu unaotekelezwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Kenya.
Takwimu za kidunia zinaonyesha mtu mmoja kati ya watu 10,000 ana tatizo la Himofilia. Mpaka sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na watu takribani milioni 56 mpaka 60 hivyo inaweza kuwa na wagonjwa wapatao 6,000 hadi 12,000. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 97 ya watu wenye ugonjwa huu duniani bado hawajagundulika ambapo kwa upande wa Tanzania waliotambulika na wanaendelea na matibabu ni 167 tu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇