CCM Blog, Dodoma
Serikali imesema Walimu wapya 6000 wa shule za Msingi na Sekondari wataajiriwa ifikapo mwezi juni, mwaka huu ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi na Walimu waliofariki au kustaafu kazi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu David Silinde Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu Swali la Mbunge wa Njombe Deodatus Mwanyika aliyetaka kujua serikali inachukua hatua ipi kumaliza tatizo la upungufu wa Walimu hasa katika shule za vijijini.
Silinde ameongeza kuwa ofisi yake inashirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kukamilisha jukumu hilo.
Mapema Naibu Waziri amesema kati ya Desemba mwaka 2015 na Septemba 2020 Serikali imeajiri Walimu 10666 wa shule za msingi na Walimu 7515 wa shule za Sekondari ili kukabiliana na upungufu uaojitokeza hususani kuwapanga katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Ameongeza kuwa kuanzia mwezi Desemba mwaka 2015 hadi Septemba 2020 Halmashauri ya mji wa Njombe imeajiri Walimu 21 wa Shule za Msingi na Walimu 111 wa Shule za Sekondari.
Silinde amesema vilevile Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa imekuwa ikifanya uhamisho wa ndani kwa kuwahamisha walimu waliozidi hasa kwenye maeneo ya mijini na kuwapanga kwenye shule zenye uhaba mkubwa wa walimu ambazo nyingi zipo maeneo ya vijijini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇