Apr 14, 2021

RC: WAKULIMA RUVUMA WAMEPATA ZAIDI YA SH. BILIONI 28 KUPITIA MFUMO WA STAKABADHI MAZAO GHALANI 2020/2021

Ruvuma, Tanzania

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema Mfuko wa stakabadhi mazao ghalani katika Mkoa wa Ruvuma umewawezesha wakulima kupata fedha zaidi ya Sh. Bilioni 28 katika msimu wa masoko wa mwaka 2020/2021.


Akifungua mkutano wa wadau wa mazao ya ufuta, soya na mbaazi uliofanyika katika ukumbi wa Songea Club, Mkuu wa Mkoa huyo wa mkoa wa Ruvuma ameyataja mazao yaliuzwa katika mfumo huo kupitia minada iliyofanyika katika wilaya za Songea,Tunduru na Namtumbo kuwa ni  ufuta, soya na mbaazi.


Mndeme, ameainisha kuwa zao la ufuta kilo ziliuzwa kilo 12,234,737 na kuwaingizia wakulima zaidi ya sh. Bilioni 25, Soya iliuzwa kilo 1,499,077 na kuwaingizia wakulima zaidi ya Sh. Bilioni moja huku zao la mbaazi zikuzwa kilo 4,260,77 na kuwaingizia wakulima zaidi ya Sh. Bilioni 2.585.


“Mfumo wa stakabadhi mazao ghalani umeonesha mafanikio makubwa katika Mkoa wetu,hivyo leo tunafanya tathmini ya msimu wa masoko uliopita 2020/2021 na kuratibu maandalizi ya msimu wa masoko wa 2021/2022 ambapo ununuzi unatarajia kuanza Mei 2021’’, alisema Mndeme.


Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amesema  mfumo huo umeziwezesha Halmashauri kukusanya ushuru kwa lengo la kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo kupitia zao la ufuta pekee zilikusanywa zaidi ya sh.milioni 954 za ushuru kwenye Halmashauri.


Mafanikio mengine ya mfumo huo ameyataja kuwa ni kufufuliwa kwa vyama vingi vya ushirika,kuongeza ajira na kwamba mfumo umerahisisha ukusanyaji wa kodi kwa ajili ya mapato ya serikali kuu kupitia Mamlaka ya Mapato tanzania (TRA).


Awali akitoa taarifa ya mazao ya ufuta,soya na mbaazi kwenye mkutano huo,Mrajisi Msaidizi wa Vyama Vya Ushirika Mkoani Ruvuma Bumi Masuba ameutaja uendeshaji wa masoko ya mazao hayo,ulifanyika kupitia vyama vya msingi 44 mkoani Ruvuma na kuleta mafanikio makubwa.


Ameyataja maandalizi ya masoko katika mkoa wa Ruvuma msimu wa 20201/2022 kuwa yanaendelea kufanyika kwa mfumo wa stakabadhi za ghalani kupitia vyama vya ushirika.


“Makadirio ya uzalishaji wa mazao hayo katika msimu huu ni ufuta tani 15,437,soya tani 7,844 na mbaazi tani 2,889’’, alisema Masuba.

********

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme  akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa mazao ya Ufuta, Soya na Mbaazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Songea Club mkoani Ruvuma.

Wadau wa mazao ya Soya, Ufuta na Mbaazi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma wakiwa kwenye mkutano uliofanyika ukumbi wa Songea Club, Ruvuma. 

Habari/Picha na Albano Midelo, Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma Aprili 13,2021

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages