Muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia umechafua ardhi kubwa ya Yemen kwa mabomu mengi ya kutega ardhini na mabomu ya vishada katika kipindi cha miaka 6 iliyopita.
Hayo yamesemwa na Kanali Ali Safra ambaye ni kamanda wa kitengo cha kutegua mabomu yaliyotegwa ardhini cha jeshi la Yemen. Safra amesisitiza kuwa, takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa, hadi katikati ya mwaka 2019, kwa uchache raia elfu sita walikuwa wameuawa kwa milipuko ya mabomu yaliyotegwa ardhini na muungano vamizi wa Saudi Arabia katika maeneo mbalimbali ya Yemen.
Afisa huyo wa jeshi la Yemen mesema, Wayemeni wako katikati ya medani iliyojaa mabomu yaliyotegwa ardhini na adui wao na kwamba, raia wengi wanashindwa kurejea katika maeneo yao yaliyokombolewa kutokana na kuwepo mabomu ya vishada katika maeneo hayo.
Kanali Ali Safra amesema kuwa, takwimu zinaonyesha kuwa, hadi sasa Saudi Arabia na washirika wake wamefanya mashambulizi 2,500 ya mabomu ya vishada katika vita vya Yemen, na tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021 karibu raia 90 wamepoteza maisha yao kutokana na mabomu hayo na makumi ya wanyama wa kufuga wameuawa.
Kamanda wa kitengo cha kutegua mabomu ya ardhi cha Yemen ameutaka Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa ziwasaidie Wayemeni kwa zana na vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kutegua mabomu hayo na kuokoa maisha ya raia wasio na hatia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇