LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 18, 2021

HALI YA MAMA JANETI MAGUFULI SIYO NZURI KIAFYA KUTOKANA NA MSTUKO ALIOPATA KUFUATIA KIFO CHA MUMEWE DK. MGUFULI

Joseph Magufuli, mtoto wa Hayati Dk. John Magufuli akizungumza kwenye Kongamano la Viongozi wa Dini kumuombea aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dk. John Magufuli lililofanyika katika Ukumbi wa Chimwaga, Dodoma, leo


CCM Blog, Dodoma

Joseph Maguli, mtoto wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli, amesema mama yake, Janeth hayupo vizuri kiafya kutokana na mstuko aliopata kufuatia kifo cha mumewe Dk. Magufuli, kilichotokea Machi 17, 2021 jijini Dar es Salaam.


Akizungumza leo Aprili 18, 2021 katika Kongamano la Viongozi wa Dini kumuombea Hayati Dk. John Magufuli lililofanyika katika Ukumbi wa Chimwaga, Dodoma, mgeni rasmi akiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Joseph amesema Mama Janet Magufuli bado anaendelea na matibabu.


“Mama hakuweza kuja kwa sababu ya tatizo la kiafya alipatwa na mstuko baada ya baba kufariki, bado anaendelea na matibabu, mama anawashukuru viongozi wa dini na watu wote kwa kuliombea Taifa wakati wote wa msiba.


Na hakika ilikuwa jambo gumu kumpoteza mzazi na kiongozi wa Taifa", ameeleza Joseph wakati akizungumza kwenye Kongamano hilo.


Pia mtoto huyo wa Hayati Dk. John Magufuli, ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kumuomba Mungu ili upendo, amani na mshikamano viendelee kutawala nchini Tanzania.


Joseph amewashukuru viongozi wa dini na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wote nchini ambao walikuwa pamoja na familia tangu walipompoteza mpendwa wao hadi maziko.


Akizungumza kwenye Kongamano hilo, Mufti wa Zanzibar, Sheikh Al Kaabi, amewataka Watanzania kuwa na utii kwa viongozi kwa kuwa wamepata bahati ya kuwa na viongozi wenye nia njema kwa ajili ya kuliongoza Taifa.


Sheikh Al Kaabi akiwasilisha mada ya utii na uzalendo kwa umoja wa Taifa, amesema ni muhimu kila mmoja ampe haki mwenzake bila kutanguliza tofauti za kidini, itikadi na ukabila.


“Ni wajibu wetu kuwatii viongozi bila kujali ukubwa wala udogo wao. Tuna bahati nzuri tumepata viongozi wenye nia nzuri na makusudio mema kwetu na Tanzania nzima.

 

Nikimzungumzia  Rais Samia Suluhu Hassan, ni kiongozi wa kwanza mwanamke, mwanamke ni mtu mwenye huruma na tunaamini Mama Samia una huruma kwa wananchi wako", alisema Sheikh Al Kaabi.


Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amesema Hayati Dk. Magufuli alikuwa na utu, alijenga uadilifu, uaminifu kwa watendaji na wafanyakazi na alikemea maovu kwa maslahi mapana ya Taifa.


“Mafunzo mengine aliyotuachia ni utu, alikuwa akiwajali watu, kuwasaidia wanyonge kupata haki zao, kuwaonea huruma lakini pia alikuwa na ukarimu kwa watu, kubwa sana na ambalo nimeona wasaidizi wake wakilifanya ni kujishusha ambayo ni silaha kubwa sana kwa nafasi uliyonayo.


Alikuwa mstari wa mbele kutatua matatizo ya watu, aliyabeba na kuyapatia ufumbuzi na pia alijenga nidhamu ya kiutendaji kwenye kila sekta.

Yeye na aliyekuwa Makamu wake wa Rais na Waziri Mkuu walifanya kazi kubwa sana ya kutatua matatizo makubwa ya nchi,” amesema Muft.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages