LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 4, 2021

WAZIRI SIMBACHAWENE ATOA WIKI MBILI KITUO CHA POLISI KIHAME


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akizungumza na Wananchi wa Mji mdogo wa Mtera, Jimbo la Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, leo, ambapo ametoa wiki mbili Kituo cha Polisi Mtera kihamishiwe katika makazi ya watu yaliyopo Barabara Kuu ya Dodoma-Iringa. Kituo hicho kipo Mtera Camp Kilomita tano kutoka katika Mji huo

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akimsikiliza Diwani wa Kata ya Mtera, Robert Maulya, alipokuwa akitoa malalamiko ya wananchi kuhusu umbali wa Kituo cha Polisi wanapoenda kuripoti matukio mbalimbali ya uhalifu. Hata hivyo, Waziri huyo ametoa wiki mbili Kituo hicho kihamishishwe Mji mdogo wa Mtera uliopo Barabara Kuu ya Dodoma-Iringa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akipokea saluti kutoka kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtera, Ally Liviga (kushoto), wakati alipokuwa anawasili katika Kituo hicho kilichopo nje ya Mji mdogo wa Mtera, Wilayani Mpwapwa, leo. Ametoa wiki mbili Kituo hicho kihamishiwe katika makazi ya watu yaliyopo Barabara Kuu ya Dodoma-Iringa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akitoka kukagua jengo lililokuwa Zahanati katika Mji mdogo wa Mtera, ambalo linatarajiwa kuwa Kituo cha Polisi Mtera baada ya Waziri huyo kutoa wiki mbili Kituo cha Polisi Mtera kilichopo mbali na makazi ya watu kihamie katika Mji mdogo wa Mtera uliopo Barabara Kuu ya Dodoma-Iringa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akiombewa na Waumini wa Madhehebu mbalimbali wa Jimboni kwake Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, kabla ya kuanza kuzungumza na Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Ipera, jimboni humo, leo. Picha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

…………………………………………………………………………………………….

Na Mwandishi Wetu, MOHA, Dodoma.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ametoa wiki mbili Kituo cha Polisi kihamishiwe katika mji mdogo wa Mtera illi wananchi zaidi ya elfu kumi wanaoishi katika Kata ya Mtera, Wilayani Mpwapwa waweze kupata huduma kwa ukaribu.

Kituo hicho ambacho kipo nje ya mji kwa umbali wa zaidi ya kilomita tano kutoka katika Mji wa Mtera ambapo ipo barabara kuu ya Dodoma kwenda Iringa, wananchi hao wamekuwa wakiteseka kwa miaka mingi kutokana na umbali wa kituo hicho wanapoenda kituoni hapo.

Waziri Simbachawene ambaye alikuwa katika ziara katika Kata hiyo, iliyopo Jimboni kwake Kibakwe, baada ya kupokea malalamiko mbalimbali ya wananchi, alifika katika Kituo hicho kilichopo katika eneo la Mtera ‘Camp’ na kuona umbali huo na pori kubwa lililopo barabarani wakati unapoelekea kituoni hapo, na akaona kuna umuhimu mkubwa wa Kituo hicho kuhamishwa.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mji huo wa Mtera, Simbachawene alisema baada ya kwenda kukikagua kituo hicho amekiona kipo porini kama wananchi wanavyosema, hivyo amesema kuna umuhimu mkubwa kituo hicho kuhamishwa.

“Kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao, kituo kipo porini, na uhalifu mwingi unatokea barabarani, wahamiaji haramu polisi wenyewe wanawakamatia hapa barabarani, wezi, wahalifu, wapiga dili na majambazi wote wanakamatiwa huku wanakoishi watu, kituo kipo mbali kabisa, porini kwasababu kilikuwa ni kambi waliorithi wakati wa ujenzi wa kituo cha Mtera zamani wakawekwa kule, hivyo Polisi wakabaki kule,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa; “Lakini hata usalama wao ni hatari sana, kwasababu nguvu ya polisi ni wananchi wake, kwasababu jeshi hili ni la usalama wa raia, polisi wakizidiwa wanawaomba wananchi muwasaidie, hivi wakivamiwa kule watasaidiwa na nani, si mtakuta wamekufa wote, na wenyewe wapo wangapi, watano, sijui sita, kule ni porini, kimsingi busara zote zinataka tufikirie upya, kituo kile kinatakiwa kihame kije huku barabarani, uamuzi wangu ni kwamba kituo kile cha polisi ndani ya siku kumi na nne kiwe kimehamia hapa barabarani.”

Hata hivyo, Waziri Simbachawene baada ya mkutano wa hadhara, alikubaliana na viongozi wa kata hiyo kuyachukua majengo yaliyokuwa Zahanati ya zamani ya Mtera yatumike kwa ajili ya Kituo cha polisi hicho pamoja na nyumba ya Zahanati hiyo ilitumike kwa ajili ya makazi ya Mkuu wa Kituo hicho.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mtera, Robert Maulya alisema kituo cha Polisi Mtera kilijengwa muda mrefu, na kilijengwa kwasababu maalumu na kwasasa kule kumekuwa porini hakuna watu zaidi ya kuwepo kwa kituo hicho pekee, hivyo kinapaswa kuhamishiwa mahali ambapo kuna wananchi kwasababu kwenda kituoni pale ni gharama pia kutokana na umbali.

“Wewe ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Polisi wapo chini yako, tunacho kituo cha polisi ambacho kimejengwa muda mrefu, na kule kilijengwa kjwa ajili ya kazi maalumu ya ujenzi wa daraja, lakini leo kule kumekuwa pori na polisi kazi zao ni kulinda raia na mali zao, sasa kule walipo, raia hawapo na mali hazipo, kwahiyo tunaomba kituo hiki kisogee hapa kijijini ili polisi hawa waweze kufanya kazi yao,” alisema Maulya.

Pia Maulya alimshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kutoa shilingi milioni 700 mwaka jana kwa ajili ya kuanzisha mradi wa maji katika Kata hiyo ambapo mpaka sasa tayari mabomba yamesambazwa kupeleka maji katika nyumba za wananchi.

Aidha, Waziri Simbachawene ametoa milioni kumi kwa ajili ya kusaidia ukarabati wa hosteli ya wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya Mtera ambayo inatarajiwa kuanza kuchukua wanafunzi hao kuanzia mwakani.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages