Na Mwandishi Maalumu, Sumbawanga
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe Omary Kipanga amesema Serikali itatumia jumla ya Shilingi bilioni 7.8 kujenga majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga kilichopo Mkoani Rukwa.
Mhe. Kipanga ameyasema hayo Mkoani Rukwa hivi karibu wakati alipokuwa anakagua eneo kitakapojengwa chuo hicho lenye ukubwa wa hekari 45 ambapo amesema chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 1,400 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 850 kulinganisha na cha awali ambacho kilikuwa kinachukua wanafunzi 550.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 tayari Shilingi bilioni 3.3 zimepitishwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo mapya ya chuo hicho kwa kutumia utaratibu wa force akaunti na kwamba ujenzi huo utaanza wakati wowote kuanzia sasa.
"Nipende kuwataarifu kuwa Serikali imejipanga kutumia Shilingi bilioni 7.8 kwa ajili ya kujenga majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga na kwamba kwa mwaka huu wa fedha tayari Sh. bilioni 3.3.zimeshaidhinishwa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo," amesema Mhe. Kipanga.
Akiongea mbele ya Naibu Waziri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nyangi Msemakweli ameshukuru Kanisa Katoliki kwa kuruhusu majengo yao kutumiwa na Serikali kwa muda mrefu na ameipongeza Serikali kwa juhudi iliyofanya kuhakikisha eneo la kujenga chuo hicho linapatikana.
Chuo cha Ualimu Sumbawanga kimekuwa kikitumia majengo ya Kanisa Katoliki tangu kianzishwe mwaka 1975 na sasa Kanisa hilo limeomba hadi kufikia mwaka 2022 kiwe kimeachiwa majengo yake kwa ajili ya matumizi mengine.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇