LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 11, 2021

WAINGIA MATATANI KISA KUSAFIRISHA NCHI ZA NJE VINYONGA NA NYOKA KIBAO

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inawashikilia Watuhumiwa watatu raia wa Tanzania  kwa kosa la kushirikiana na raia wa Jamhuri wa Czeck kusafirisha nje ya nchi vinyonga 74 na nyoka 6 kinyume na sheria.


Akizungumza na Vyombo vya habari leo mkoani Iringa, Waziri wa Maliasili na Utali, Dkt.Damas Ndumbaro amesema vinyonga na nyoka hao walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Vienna na Maafisa wa Forodha wa Austria wakiwa kwenye begi ambalo ndani yake waliwekwa kwenye soksi na kuingizwa kwenye vifungashio (container) vya plastiki.


Amesema Watuhumiwa hao  wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani kesho ambapo watakabiliwa  na makosa ya kusafirisha nje Wanyamapori hao bila kibali, Uhujumu uchumi pamoja na utakatishaji fedha kupitia Biashara hiyo.


 Dkt.Ndumbaro amesema vinyonga na nyoka hao inadaiwa  wametoka Tanzania katika Milima ya Usambara ambako kuna aina mbalimbali za vinyonga.


Akizungumzia jinsi Watuhumiwa hao walivyonaswa,  Waziri wa  Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amesema baada ya kupata taarifa kupitia mitandao ya kijamii, Wizara kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama na kwa kutumia Kikosi Kazi Taifa Dhidi Ujangili iliunda Kikosi Maalum cha kuchunguza tukio hilo.


Amesema kupitia  taarifa za Kiintelijensia Kikosi Maalum kilifanikiwa kupata jina la mtuhumiwa aliyesafirisha vinyonga hao ambaye  raia wa Jamhuri ya Czeck.


Hata hivyo, amesema uchunguzi bado unaendelea sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubaini namna vinyonga na nyoka hao walivyopitishwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere bila kugundulika. 


Amesema Watuhumiwa watakaobainika kuhusika na uhalifu huo wataunganishwa na wenzao ambao tayari wamekamatwa. 


Pamoja na juhudi hizo, Waziri Dkt.Ndumbaro amesema  Serikali  ya Tanzania  itashirikiana na nchi ya Austria katika uchunguzi unaoendelea ikiwa ni pamoja na kuwarudisha Tanzania vinyonga pamoja na nyoka  hao. 


Aidha, Amesema Serikali itawasiliana na Jamhuri ya Czeck ili watuhumiwa hao ambao ni raia wake  wachukuliwe hatua.


Katika hatua nyingine , Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro amesema Serikali  inakusudia kuifuta kabisa Biashara ya  wanyamapori hai ambayo ilizuiwa tangu mwezi Mei, 2016.


Amesisitiza kuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kufanya biashara ya wanyamapori hai ndani na nje ya nje ya  nchi na Mtu yeyote atakayebainika kufanya biashara hiyo wakati imezuiliwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages