Wakati wakiwasilisha malalamiko yao walidai kuwa Mkurugenzi huyo amewatolea lugha ya kuwadhalilisha baada ya madiwani hao kumhoji juu ya mapato na matumizi ya halmashauri katika kikao cha kisheria cha kamati ya fedha na mipango ambapo zaidi ya Shilingi Milioni 120 zikiwa hazijulikani matumizi yake na kuongeza kuwa majibu ya mkurugenzi huyo yalikuwa madiwani hao hawana mamlaka ya kumhoji.
Msafara huo wa madiwani waliofika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Apolinary Macheta, Mbunge wa jimbo la Kwela Mh. Deus Sangu Pamoja na madiwani wa kamati ya Fedha na Mipango ambao kwa Pamoja walimfikishia Mkuu huyo wa mkoa maamuzi ya kutoendelea kufanya kazi na Mkurugenzi wao.
Akitoa ufafanuzi wa tukio hilo Mh. Macheta alisema, “Tumekwenda kwenye agenda inayohusiana na fedha za matumizi ya ununuzi wa gari, Halmashauri tulitenga milioni 92, lakini baadae zikatoka milioni 32 kupitia baraza kwaajili ya kwenda kuhudumia ule mradi wa stendi zikabaki milioni 60, sasa zile milioni 60 wajumbe wakahoji, hizi fedha mbona mnatuletea hapa kanakwamba zilishatumika kwenye kabrasha zinaonekana, Mkurugenzi aliposimama akasema mimi mwenyewe sijui aliyezitumia,”
“Hapa nilimwachia ofisi afisa mipango niliporudi nikakuta zimeshatumika, kwahiyo wa kumhoji ni afisa mipango na sio mimi, wajumbe wakasema wewe ndio mkurugenzi kwanini tumhoji mtu mwingine, mkuu wa idara wakati wewe ndiye afisa masuhuli, nimesema siye niliyezitumia aliyezitumia ni afisa mipango ndio mumuhoji, yaani kwa ukali,” Alielezea.
Aidha, Mbunge wa jimbo la Kwela lililopo katika halmshauri hiyo mh. Deus Sangu alieleza kuwa ni mara yake ya kwanza kushiriki katika vikao hivyo lakini hali aliyokutana nayo hakuitarajia.
“Mimi binafsi ndio kilikuwa kikao cha kwanza kukutana na Mkurugenzi yaani nilikuwa ‘dissapointed’ sana, sikudhani vikao ‘official’ na ‘formal’ kama vile angeweza ‘ku-react’ mbaya Zaidi ameenda kuituhumu kamati ya LAAC, kwamba mimi sitishwi na lolote hata hao LAAC walikuja wakapoa wenyewe, walikuja kunitaka niwape rushwa bilioni 10 nikawakatalia lakini baadae wameniacha hata huyo CAG alitaka kuja kukagua huku ameahirisha kuja kwa maelekezo ya Rais, sasa wewe kama mbunge unahoji, unahoji nini?” Alisisitiza.
Akiongeza maneno yaliyosemwa na wajumbe wengine Diwani wa Viti Maalum Umulina Mgawe alisema kuwa mkurugenzi huyo amekuwa akijipangia ratiba za vikao vya kamati hizo huku akiwa na visingizio mbalimbali pale anapohojiwa juu ya tarehe za vikao hivyo.
“Ukweli kabisa mwenyekiti anavyoeleza ni sahihi kabisa na wote tulikuwa humo na sisi tukaamka tukamwambia mkurugenzi, usitunyanyase, huu udiwani tuna maisha yetu hata hapo baadae, sisi ni wawakilishi wa wananchi, kwanini unatufanyia hivyo mbele ya wakuu wa Idara, ukweli tulinyanyasika, mheshimiwa mbunge baada ya kuona hali ilivyo mule alianza kukusanya vifaa na kuondoka, mimi nikamwambia mkurugenzi usidhani kwamba mheshimiwa anakwenda kwenye njia ya msalaba kama alivyosema yaani hali imemshinda,” Alielezea.
Halikadhalika katika kufafanua hilo Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule ambaye aliwakilishwa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo katika kikao hicho alithibitisha kuwepo kwa sintofahamu hiyo ndani ya kikao baada ya kupewa taarifa ya mwenendo wa kikao kilivyokuwa mara tu baada ya kikao hicho kumalizika.
“Wajumbe walifanya ziara na mkurugenzi aliandaa taarifa na ikaonesha kuna vifaa vya Shilingi milioni 17 vimepotea, kwahiyo wajumbe wakataka kujua hivyo vifaa vimepotea poteaje nah atua zilizochukuliwa na ‘reaction’ ya Mkurugenzi ndio ilikuwa hiyo kwamba wao hawana mamlaka ya kumhoji, yeye ameteuliwa na Mheshimiwa Rais na kwamba anawajibika kwake na hawajibiki kwa waheshimiwa madiwani,” Alisema.
Kwa upande wake Mh. Wangabo amesikitishwa na kitendo hicho na mkurugenzi huyo kuwadhalilisha madiwani hao na kusisitiza kuwa hakuna haja hoja moja iliyohojiwa na na madiwani hao ambayo imekwenda kinyume na ufuatiliaji wa maendeleo ya wananchi na kuongeza kuwa mkurugenzi huyo hakuwa na sababu ya kuongea maneno aliyoyaongea ya kujihusisha kuwa mwenye mamlaka pekee ya kumhoji yeye ni Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
“Waheshimiwa hawa madiwani wa Halamshauri ya Wilaya ya Sumbawanga hawawezi kufanya kazi na yule Mkurugenzi, lakini niende mbali Zaidi, si kwamba anakataa au hana ushirikiano na madiwani hiyo lakini pia hata Katibu tawala wa mkoa huu hakuna ushirikiano nay eye, suala hili lilikuwa ni zito na tukalichukulia hatua, sasa huyu mkurugenzi hataki kufanya kazi na madiwani wake, na wakati huo huo hataki kutoa ushirikiano kwa katibu tawala wa mkoa, sasa yeye ni nani?”
“Kwa hali hiyo niwaombe sana waheshimiwa madiwani, mheshimiwa Mbunge endelezeni ukomavu na utulivu mliouonesha, endeleeni nao huo, niwasihi sana mfanye kazi, kazi hizi ni za wananchi na ninyi mmechaguliwa na wananchi, sasa huyu mtu mmoja asitukwaze, tutachukua taratibu, sheria na miongozo ambayo ipo, tutaieleza mamlaka yake ya nidhamu ili ichukue hatua stahiki,” Alisisitiza.
Hoja alizoulizwa mkurugenzi huyo ni Pamoja na kutoa maelezo ya upotevu wa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 17 kwenye hospitali ya Wilaya, kutoa maelezo ya matumizi ya fedha iliyotengwa kwaajili ya kumalizia stendi ya mabasi katika mji mdogo wa Laela shilingi milioni 32, kutoa maelezo ya matumizi ya shilingi milioni 45 ya fedha za mapato ya ndani katika Uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba, 2020, kutoa maelezo ya fedha shilingi milioni 60 zilizotengwa kwaajili ya ununuzi wa gari, Pamoja na kutoa maelezo ya fedha za ujenzi wa ofisi ya mkurugenzi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇