Ijumaa ya juzi tarehe 26 Machi, vita na mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen viliingia katika mwaka wake wa 7.
Baada ya kupita miaka 6, kuashiria mambo ambayo ni uhakika kuhusu vita hivyo ni jambo lenye umuhimu mkubwa.
Uhakika wa Kwanza; ni kwamba, katika dunia ya leo haiwezekani kuanisha nguvu za nchi fulani kupitia vita dhidi ya nchi nyingine. Jambo hili ni tofauti na masuala ya ndani ya nchi, kwani mapigano ya ndani ya nchi endapo yatashadidi inaweza kuwa sababu ya kubadilisha uongozi na madaraka ya nchi. Jambo hilo lilishuhudiwa mwaka 2011 katika nchi za Tunisia, Misri, Libya na hata nchini Yemen, licha ya kuwa, machafuko ya ndani katika nchi hizo hayakuwa ya aina moja.
Ilikuwa Machi 26 mwaka 2015, wakati Saudia ikipata himaya na uungaji mkono wa Marekani na kwa ushiriki wa nchi kama Imarati na nyinginezo, ilipoanzisha hujuma na mashambulio yake ya kijeshi kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdurabuh Mansur Hadi na kuiondoa katika ulingo wa madaraka Harakati ya Ansarullah. Hata hivyo, hivi sasa imepita miaka 6 na Saudia na waitifaki wake wameshindwa kufikia malengo yao. Si hayo tu, bali Ansarullah ya Yemen na washirika wake ndio iliyoweza kuunda serikali na leo harakati hiyo inahesabiwa kuwa nguvu muhimu ya kisiasa nchini Yemen.
Uhakika wa Pili; ni kwamba, muungano vamizi unaoongozwa na Saudia katu haujaweza kuwa na umoja na mshikamano. Licha ya kuwa, Saudia ilianza mashambulio dhidi ya Yemen ikiwa na nchi 10 zinazoiunga mkono, lakini baadaye muungano huo ulisambaratika. Aidha hata uwepo wa pamoja wa Saudia na Imarati katika vita hivyo haukuwa na malengo mamoja.
Hii leo Saudia na Imarati hazina daghadhagha na hangaiko moja katika kadhia ya Yemen. Kabla ya kila kitu, Imarati inafuatilia suala la kuwa na satua na ushawishi katika maeneo ya kusini mwa Yemen na kuimarisha nafasi yake katika eneo. Saudia kwa upande wake inakabiliwa na vitisho vya ndani vinavyotokana na mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani za Wayamen, na inachoshughulishwa nacho kwa sasa ni kuzuia isipate pigo kubwa zaidi katika vita hivyo. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Saudia inaamini kwamba, kuhitimishwa vita hivi sasa huko Yemen hakuendani na maslahi yake kwani haionekani kama ni mshindi wa vita hivyo.
Kuhusiana na hilo, Sayyid Abdul-Malik Badruddin al-Houthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen, alitangaza Alkhamisi iliyopita sambamba na kutimia miaka sita ya vita hivyo kwamba, licha ya ukweli na uhakika wote kudhihirika wazi, lakini Saudia bado tu haijapata funzo.
Uhakika wa Tatu; ni huu kwamba, utawala vamizi wa Saudia ndio mshindwa mkubwa zaidi wa vita huku utawala haramu wa Israel ukiwa ndio mshindi mkubwa wa vita dhidi ya Yemen. Saudia sio tu kwamba, imeshindwa kutekeleza madai yake kwamba, itaibuka na ushindi katika vita hivyo katika muda wa wiki mbili, bali baada ya kupita miaka sita tangu kuanza vita hivyo, imezama na kunasa katika kinamasi cha vita hivyo.
Hii leo Saudia ina hofu kubwa na mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani za Wayamen dhidi yake na kwa namna fulani udhaifu wa dola hilo la Kiarabu umedhihirika bayana. Haya ni mambo yanayokinzana wazi kabisa na madai kwamba, Saudia ni dola lenye nguvu katika eneo la Asia Magharibi. Vita dhidi ya Yemen vimetilia alama ya swali nguvu na uwezo wa Suadia.
Mkabala na hilo, utawala haramu wa Israel ndio mshindi mkuu wa vita hivyo, kwa sababu katika upande mmoja, umeshuhudia vita vya nchi ya Kiislamu dhidi ya nchi nyingine ya Kiislamu na katika upande wa pili, umekuwa mshirika na Saudia katika anuani ya "muuaji wa watoto".
Katibu Mkuu wa Ansarullah ya Yemen anaamini kuwa, kuamini kibubusa Saudia na Imarati tathmini na ripoti za mashirika ya kijasusi ya Israel na Marekani katika kumtambua adui pamoja na harakati zake, ndio sababu ya kuchukua maamuzi yasiyo sahihi.
Hivyo tunaweza kusema kuwa, vita dhidi ya Yemen ni mtego ambao uliwekwa na mashirika ya kijasusi ya Marekani na Israel kwa ajili ya Saudia.
Uhakika wa Nne; ni kuwa, Umoja wa Mataifa na madola makubwa ya dunia, nayo ni washindwa wakuu wa vita vya muungano vamizi Saudia dhidi ya Yemen. Licha ya kukiri bayana Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba, Yemen inakabiliwa na maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika karne ya 21 ikiwa ni taathira ya vita, lakini asasi hiyo ya kimataifa haijachukua hatua yoyote ile ya maana ya kusitisha vita hivyo. Si hayo tu, bali Umoja wa Mataifa umeshindwa kutoegemea upande wowote katika vita hivyo. Kila mara Wayamen walnapoonekana kupata ushindi, basi Umoja wa Mataifa ndipo nao unapoongeza juhudi zake za kisiasa.
Abdul-Malik al-Houth anasema kuhusiana na hilo kwamba, kila mara muungano vamizi wa Saudia ulipokabiliwa na hali ngumu, kimaadili, katika medani na kisiasa, Umoja wa Mataifa huingilia kati na kuwaambia Wayamen wasitishe vita. Mbali na Umoja wa Mataifa, madola ya Magharibi nayo ni washindwa wa vita dhidi ya Yemen. Hata kama madola hayo yameweza kunufaika kiuchumi kwa kuiuzia silaha Saudia, lakini imethibiti mbele ya fikra za waliowengi ulimwenguni kwamba, suala la haki za binadamu ni madai matupu tu kwa madola hayo, kwani licha ya Yemen kukabiliwa na maafa ya kibinadamu hayajashughulishwa kabisa na suala la kuhitimishwa vita hivyo au kusitisha himaya na uungaji mkono wao kwa Saudia.
Uhakika wa Tano; ni kuwa, wananchi madhulumu wa Yemen ndio wahanga wakuu wa vita hivyo visivyo vya kiadilifu. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Yemen zilizotolewa mwishoni mwa miaka sita ya vita hivyo ni kuwa, zaidi ya watu 43,000 wameuawa au kujeruhiwa. Aidha takribani watu milioni 4 wamelazimika kuwa wakimbizi. Magonjwa na njaa ni maumivu makubwa mawili ambayo yanawakabili wananchi wa Yemen. Yote hayo yakiwa ni matokeo ya vita vya Saudia na washirika wake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇