LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 28, 2021

KHERI JAMES : TUTAMPA USHIRIKIANO WA KUTOSHA RAIS MAMA SAMIA

 


Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Kheri James,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 28,2021 jijini Dodoma

Na.Alex Sonna,Dodoma
Tunakwenda na Mama!Tunamuunga  Mkono Mama! Ni kauli ya Umoja wa vijana  wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umeahidi kumpa ushirikiano wa bega kwa bega Rais Samia Hassan Suluhu huku ukimpongeza  kwa kuteuliwa kwake Katika nafasi hiyo kwa mujibu wa katiba .

Kauli hiyo imetolewa leo Machi 28,2021 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa UVCCM, Taifa, Kheri James,wakati akizungumza na waandishi wa habari,amesema kuwa wao kama vijana watatoa ushirikiano Mkubwa Kwa Rais Mama Samia ili kuleta maendeleo katika nchi yetu kwa kufuata katiba na Ilani ya CCM.

Aidha Bw.James amewatoa  hofu vijana na watanzania kuwa licha ya kumpoteza kiongozi shupavu, Dk John Magufuli ambaye alifariki Machi 17 mwaka huu lakini uwezo alionao Mama Samia ni mkubwa na anatosha kuvaa viatu vya Dk Magufuli katika kuwatumikia watanzania.

“Tuna Imani na Mama Samia kwa kuwa tumefanya nae kazi na tunatambua kuwa yeye ni mlezi kwa vijana hivyo niwatoe wasiwasi vijana nchini ambao wanawaza Dkt Magufuli hayupo hali itakuwaje ,huyu Mama ataendelea kuwa mtetezi wetu,”amesema Kheri James.

Bw.James amesema ikumbukwe Mama Samia alipokuwa Makamu wa Rais alikuwa muumini wa kuwashirikisha Vijana kwenye mambo mengi ya Msingi hivyo kwa sasa atatuvusha zaidi na sisi tunaahidi kudumisha mshikamano na pia tunawataka watanzania wote kumuunga mkono kwa kushikamana na kufanya kazi.

” Sasa ni jukumu letu  vijana ni kuhakikisha tunaisimamia dhamira aliyonayo Rais wetu Mama Samia ya umoja na mshikamano na sisi tuna wajibu wa kumuunga mkono, tusiwe sehemu ya chuki na kama huko nyuma kuna mahali tulikwazana tunaomba radhi lengo liwe kutengeneza jukwaa safi la Rais wetu katika kuwatumikia watanzania.

Hivyo natoa wito kwa vijana wa CCM na vyama vingine kumrahisishia kazi Rais wetu ili asonge mbele, tunaweza kutofautiana kwenye itikadi lakini linapokuja suala la umoja tushikamane na kuitumikia wote nchi yetu,” Amesisitiza Bw. James.

Hata hivyo amewatoa hofu vijana kuwa yale yote yaliyoahidiwa kwenye kampeni na Dk Magufuli yataendelea kutekekezwa na Rais Mama Samia na yeye kama muwakilishi wa vijana ataendelea kusimamia na kukumbusha ahadi zote zinazowahusu vijana ili ziweze kutimizwa.

” Ni kweli tumempoteza kiongozi wetu Dk Magufuli niwatoe hofu kilichokufa ni kiwiliwili chake tu ila fikra na misingi ya kazi aliyoitengeneza itaendelea kudumu kwa miaka mingi zaidi, tuna imani kubwa kama vijana na uongozi wa Mama Samia tuliona uwezo na kasi yake akiwa Makamu hatuna shaka nae na sisi kama vijana tunamuahidi tupo nae bega kwa bega,” Amesema Kheri James.

Aidha Mwenyekiti huyo wa UVCCM Taifa ametoa pongezi  kwa Abdul Nondo ambaye kwa kipindi kirefu ameonyesha kuwa kinyume na mambo yanayofanywa na Serikali lakini kwa kipindi hiki yupo bega kwa bega katika kuwahamasisha vijana wengine kumuenzi Hayati Magufuli.

Katika hatua nyingine ameeleza kuwa uongozi wa UVVCM unatarajia kukutana kujadili namna bora ya kumuenzi Hayati Magufuli kutokana na mengi aliyoyafanya kwa watanzania.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages