LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 5, 2021

CCM TABORA YAOMBA WAZAWA KUPEWA KIPAUMBELE KWENYE MIRADI MIKUBWA YA UJENZI WA BARABARA

Na Tiganya Vincent, Tabora                               

KAMATI ya siasa Mkoa wa Tabora ya  Chama cha Mapinduzi (CCM) imeiomba Serikali kutoa kipaumbele kwa Wakandarasi wazawa katika eneo husika kwenye miradi ya ujenzi pindi inapotangazwa ili kuwaimarisha kimitaji na uwezo na kuimarisha uchumi wa eneo husika.


Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi wakati alipongoza  wajumbe wenzake Kamati ya Siasa kukagua ujenzi wa  barabara ya Urambo hadi Urambo yenye urefu wa Kilometa  28 iliyojengwa na Kampuni ya SAMOTA.


Alisema Wakandarasi wazawa ambao wanaonyesha uwezo na uaminifu katika utekelezaji wa miradi ikiwemo ya ujenzi wa barabara pindi zabuni zinapotangazwa zabuni na wao kuomba wapewe upendeleo kwa ajili ya kuwajenga na kuwaimarisha zaidi ili wakue na kuweza nao kuomba kazi nje ya Nchi.


Wakasuvi alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama ya mradi kwa Serikali kwa kuwa Mkandarasi wa eneo husika hakutakuwa na gharama kubwa za usafishaji wa mitambo kutoka mbali.


“Tunaomba kutoa kipaumbe kwa wazawa ili tuwe na faida nyingi ikiwemo kuwaimarisha kimitaji , ujuzi na pia hata fedha wanazopata zitabaki hapa nchini na kutoa ajira nyingi kwa wataalamu wetu wa ndani “ alisisitiza.


Aidha Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya Shina hadi Mkoa na wananchi wote kuwa walizi wa miundombinu inayojengwa kwa kuwafichua wizi wa alama za barabara ili iweze kuwa rafiki wa watumiaji.


Alisema ung’oaji wa alama hizo umekuwa ikirudisha nyuma juhudi kubwa za Serikali na kuongeza lazima wahalifu wafichuliwe na kuchukuliwa hatua kali ili kudhibiti uovuo huo.


Mkurugenzi wa Kampuni ya SAMOTA Salumu Abdallah aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwaamini wazawa na kuwapatia miradi ya ujenzi wa barabara kubwa ikiwemo wao ambao wanajenga barabara ya kutoka Urambo hadi Kaliua kwa gharama ya shilingi bilioni 38.7.


Alisema hatua hiyo imewasaidia sana kuwajengea uwezo na kupata ujuzi kutoka Mshauri Msimamizi ambapo hivi sasa wana uwezo wa kufanya kazi nyingine kubwa za ujenzi wa barabara kutokana mafunzo wayopata.


Abdallah alisema ni vema Serikali inapokuwa na miradi ikaweka utaratibu wa kutenga miradi ambayo wazawa wanapaswa kujenga kwa kuwa wao hawana uwezo wa kushindana kwenye zabuni na Kampuni za nje ya Nchi kutokana na mitaji yao kuwa kidogo ukilinganisha na wageni.


Kwa upande wa Meneja wa Mkoa wa Tabora wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Damian Ndabalinze alisema kuwa barabara hiyo ya kutoka Urambo hadi Kaliua imekamilika kwa kiwango kikubwa zilizobaki ni kazi ndogo ndogo ambazo zinatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.


Alisema baadhi ya shughuli zilizobaki ni pamoja na mifereji ya maji ya mvua, kuweka alama za kuvuka watu, kuweka mawe yanayoonyesha umbali, na kuchora michoro ya usalama barabarani .


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi (wa pili kulia)  akitoa maoni yake jana wakati alipongoza  wajumbe wenzake Kamati ya Siasa kukagua ujenzi wa  barabara ya Urambo hadi Urambo yenye urefu wa Kilometa  28 iliyojengwa  na Kampuni ya SAMOTA

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages