Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahimu Juma akimuapisha aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu jijini Dodoma, leo. Uapisho huo umefanyika mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Ikulu, Chamwino, Dodoma
Aliyekuwa Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango leo ameapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino jijini Dodoma.
Baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Dk. Mpango amemshukuru Rais Samia kwa kumchagua na kusema kwamba hakuwahi kuota kushika nafasi hiyo ya Makamu wa Rais na kumuomba Rais kumtuma wakati wowote hata ikiwa saa sita usiku.
“Mimi mtoto wa maskini sikuota kushika nafasi hii, nakuahidi nitatekeleza kwa bidii kazi zote utakazo nituma nakuomba unitume nitume hata saa sita usiku na Mchana ili kufanikisha Ilani ya CCM pia nitatekeleza Katiba kama ilivyoelekezwa kwenye ibara ya 40, na katika kutekeleza majukumu hayo yote nitashirikiana na viongozi wote wa pande zote mbili za muungano, mihimili yote mingine na zaidi viongozi wengine.” Amesema Dkt Mpango na kuongeza;
“Nishukuru pia Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kwa kulipitisha jina langu, nawashukuru pia Wabunge wote kwa kuniamini na kunichagua kwa kura zote 363 sawa na 100%, niwashukuru pia wananchi wangu wa Buhigwe kwa kunipa imani yao kwa kunichagua tena kwa kura nyingi za kishindo, natoa shukrani za dhati kwa Wizara ya Fedha.
Dk. Mpango amechukua nafasi hiyo baada ya kuachwa wazi na aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye amechukua kiti cha Urais kwa mujibu wa Katiba kufuatia aliyekuwa Rais Dk. John Magufuli kufariki Dunia Machi 17, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇