Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abei jijini Arusha, leo Februari 9, 2021. Picha zaidi chini ya habari.
Na Mwandishi Maalum, Arusha
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Jumanne, Februari 9, 2021 amefungua Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi yanayoendelea katika Viwanja vya Shiekh Amri Abied jijini Arusha.
Katika ufunguzi huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza mifuko na programu zote za uwezeshaji zifanye tathmini ya shughuli na huduma zake ili kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji uboreshaji hususan eneo la masharti ya utoaji mikopo kwa wajasiriamali.
Pia, Waziri Mkuu ameitaka mifuko inayotoa dhamana kwa wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali nchini, iimarishe usimamizi, uratibu na utendaji wake kwa kutengeneza mipango maalum ya kila mwaka inayoonesha malengo ya dhamana zitakazotolewa katika mwaka husika.
Amesema mipango maalumu itakayoandaliwa na mifuko inayotoa dhamana kwa wafanyabiashara na wajasiriamali inatakiwa iwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na baadaye taarifa za utekelezaji zitolewe katika kipindi cha kila robo mwaka.
“Wasimamizi na Watendaji wa mifuko na programu pamoja na walengwa jiepusheni na vitendo vya rushwa kwani rushwa ni adui wa haki na ni kikwazo kikubwa cha maendeleo. Pia, watendaji wa mifuko na programu za uwezeshaji pamoja na taasisi za fedha hakikisheni mnatoa huduma bila urasimu wala ubaguzi wa aina yoyote. Nasisitiza wananchi wanapofika kwenye ofisi zenu wapokelewe kwa staha, wasikilizwe na kupatiwa huduma stahiki kwa wepesi.”
Aidha, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri nchini zihakikishe zinatenga asilimia 10 ya mapato yake ya fedha za ndani ili zitumike kutoa mikopo kwa vijana (asilimia 4), wanawake (asilimia 4) na watu wenye ulemavu (asilimia 2). Pia, ametoa wito kwa Mabaraza ya Madiwani katika kila Halmashauri kufuatilia utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali ambayo yameridhiwa na Bunge na kutungiwa sheria mahsusi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu bidhaa mbalimbali wakati alipotembelea Banda la Fabiola Panga kutoka wilayani Hanang Mkoa wa Manyara (kulia) katika Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, leo. Wa Pili kushoto ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’i Issa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama sabuni na bidhaa mbalimbali za usafi majumbani wakati alipotembelea banda la Joyce Mizambwa (kushoto) katika Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, leo. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwira.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu bidhaa mbalimbali alipotembelea banda la Jonia Kalumuna katika Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, leo. Wa pili kushoto ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’i Issa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mazuria yaliyofumwa kwa kutumia nyuzi za pamba alipotembelea banda la Lucas Saguda katika Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, leo (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇