Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Ruvuma Kamishina msaidizi wa Polisi Simon Maigwa Marwa wa pili kulia akiwaonesha waandishi wa Habari(hawapo pichani)silaha aina mbalimbali zaidi ya 160 zilizokamatwa kwenye hifadhi na mapori ya akiba mkoani Ruvuma kufuatia msako mkali unaofanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na kikosi cha kuzuia ujangili kanda ya kusini, ambapo jumla ya watuhumiwa 68 wamekamatwa katika misako hiyo inayoendelea, kwanza kulia kamanda wa kikosi cha kuzuia ujangili kanda ya kusini Keneth Sanga. (Picha na Muhidin Amri). …………………………
Na Muhidin Amri,Songea
JESHI la polisi mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na kikosi dhidi ya ujangili na pori la akiba Liparamba chini ya Mamlaka ya usimamizi wa wanyama Pori Tanzania(TAWA) kanda ya kusini wamekamata silaha 160 aina mbalimbali.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Kamishina msaidizi wa Polisi Simon Marwa amesema,mbali na silaha hizo pia wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 68 waliokutwa wakifanya matukio ya ujangili kwenye hifadhi na wengine wakimiliki silaha kinyume cha sheria.
Alisema, kukamatwa kwa silaha hizo kumefuatia misako mikali dhidi ya silaha halamu na watu wanaojihusisha na vitendo vya uharifu na ujangili unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.
Kamanda Maigwa ametaja silaha hizo ni Magobole 149,Rifle 3 na ShortGun 8 ambazo alisema, kama silaha hizo zingeendelea kuwepo mikononi mwa waharifu zingesababisha madhara mbalimbali ikiwemo kuua wanyamapori na kufanya ujambazi na makossa mengine yanayohusiana na matumizi ya silaha.
Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa,silaha hizo zitaendelea kuteketezwa kufuatia taratibu za kisheria za uteketezaji wa silaha halamu ili zisilete madhara kama ilivyoelezwa na zile zinaunganisha na watuhumiwa zitatumika mahakamani kama sehemu ya vielelezo.
Aidha kamanda Maigwa ametoa rai kwa wananchi wanaomiliki silaha kinyume na sheria kuzisalimisha haraka kabla ya mkono wa sheria haujawafikia.
Kwa upande wake kamanda wa kikosi cha kuzuia ujangili kanda ya Kusini Keneth Sanga alisema,wamejipanga vyema katika kukabiliana na vitendo vyote vya ujangili na majangili kwenye hifadhi na mapori ya akiba na kuwaonya watu kuacha vitendo hivyo kwani vinaweza kuwapeleka mahali pabaya ikiwemo kupoteza maisha yao.
“kikosi chetu cha kuzui ujangili kanda ya kusini kimejipanga vyema kukabiliana na watu na matukio yote vya ujangili,nawaonya watu wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni hatari kwa usalama na maisha yao”alisema Sanga.
Alisema,silaha hizo zilizokamatwa zimeokoa maisha ya wanyama wengi ambao ni kivutio cha utalii kwa kizazi cha sasa na baadaye na kuwataka raia wema kutoa ushirikiano kwa kikosi hicho na kuwafichua watu wanafanya vitendo vya ujangili.
Aidha alisema, katika kutekeleza majukumu yake kikosi cha kuzui ujangili kimekuwa kikishirikiana na wadau wengine kwa kutoa elimu ya uhifadhi kwenye maeneo yote yanayozunguka hifadhi ili kuzui madhara ya wanyama dhidi ya wananchi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇