Na Catherine Sungura, WAMJW-Mwanza
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya huduma za Saratani lenye ghorofa tatu katika hospitali ya rufaa ya kanda Bugando ili kuweza kusogeza huduma za saratani kwenye mikoa nane ya kanda ya ziwa .
Akiongea kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo ambalo litagharimu shilingi bilioni 5.4.
Dkt. Gwajima amesema jengo hilo kitasaidia kupanua huduma za saratani nchini hususani kanda ya ziwa pamoja na kuwapunguzia muda wakazi wa kanda ya ziwa ambapo awali huduma hizo zilikua zikipatikana jijini Dar es Salaam kwenye Taasisi ya Saratani ya Ocean raod na hivyo kudidimiza uchumi wa wana familia wengi.
“Dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ni kuimarisha huduma za afya kwenye maeneo mengi nchini hususan kuboresha huduma za Saratani kwenye hospitali za rufaa za kanda ili kuhakikisha anawapunguzia kero za kufuata huduma hizi jijini Dar es salaam ikiwa ni pamoja na kudhibiti ugonjwa huu kwa kufuata mtindo bora wa maisha”.Alisema Dkt. Gwajima.
Aidha,Dkt. Gwajima amesema jengo linalojengwa kwa mfumo wa ujenzi shirikishi (force account) litakuwa na ghorofa tatu na litakapokamilika litakuwa na vitanda 120 vya kulaza,sehemu ya mionzi tiba,eneo la kupumzika baada ya kupata mionzi, ushauri, matibabu na wodi ya kulazwa wagonjwa .
“Niwapongeze Bugando kwa utaratibu wa ujenzi mlioutumia kwani mmeweza kupunguza gharama za uzalishaji kwani mmesaidia kudhibiti matumizi ambapo msingetumia utaratibu huu jengo hili lingegharimu shilingi bilioni 7 na zaidi lakini sasa litatumia bilioni 5.4,hongereni sana kwa maamuzi haya Bugando”.
Hata hivyo Dkt. Gwajima hakusita kutoa elimu kwa wananchi waliofika kwenye viwanja vya hospitali hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ambapo aliwataka wananchi kudhibiti magonjwa hayo kwa kubadilisha mtindo wa maisha,kufanya mazoezi,kutokuvuta sigara,kunywa maji mengi, kutokunywa pombe kupitiliza na uzito mkubwa.
“Wananchi lazima waelewe na kuwa na mfumo mzuri wa maisha kwa kufuata mtindo bora wa maisha na kujenga mazoea ya kwenda kwenye vituo vya afya kufanya uchunguzi wa afya zetu ili endapo upo kwenye hatua ya awali uweze kutibiwa mapema na kuishi maisha yako ya kawaida,ila ukichelewa itaenda kwenye hatua ya tatu na ya nne ambayo ni ngumu kuzuilika".Alisisitiza Dkt. Gwajima
Aliongeza kuwa magonjwa yasiyo ambukiza kama presha,moyo , kisukari na mengine yanaweza kuzuilika kwani Mwenyezi Mungu amewapa maarifa watu wake hivyo kila mmoja anatakiwa kutekeleza yale yote wanayoelekezwa na wataalam kwa kuwa siri ya kudhibiti magonjwa yapo kwenye maarifa ambayo yalitolewa na mababu kwa kutumia tiba asili.
Dkt. Gwajima amewasisitiza wataalam wa afya kuzidi kutoa elimu ya afya kwa umma kila eneo la nchi ili kila mtanzania kuwa na utamaduni mzuri wa kuzuia magonjwa kwani mwili utakua na askari imara wa kuzuia magonjwa.
Katika kuadhimisha siku ya saratani dunia,hospitali ya rufaa ya kanda bugando imefanya uchunguzi wa saratani kwa wakazi wa mwanza kwa siku mbili upande wa saratani ya tezi dume, matiti na shingo ya kizazi, jumla ya watu 217 wamepata huduma hiyo bila malipo na jumla ya watu waliogundulika kuwa na viashiri vya saratani na wameshauriwa kuanza huduma za vipimo katika hospitali hiyo ili kupata tiba sahihi shingo ya kizazi (14), matiti(11) na tezi dume (0).
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akizindua ujenzi wa jengo hilo akiwa pamoja na viongozi wa Kanisa, Mkoa na hospitali hiyo jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇