Na CCM Blog, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Generali Wilbert Ibuge, leo amefanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini India Baraka Luvanda, katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mji wa Serikali wa Mtumba, jijini Dodoma.
Mazungumzo hayo yalilenga kubadilishana mawazo na uzoefu baina yao kuhusu masuala mbalimbali hususan katika kudumisha na kuboresha uhusiano na ushirikiano uliopo katika ya Tanzania na India, kutangaza fursa zilizopo Tanzania ili kuvutia zaidi biashara na uwekezaji nchini kutoka India.
Jitihada za kutangaza fursa zinazopatikana nchini zimekuwa zikiendelea kufanywa na Wizara, kupitia Balozi zake ikiwa ni utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya Rais Dk. John Magufuli ya kuhakikisha kuwa Diplomasia ya Uchumi inatekelezwa ili kuinufaisha nchi kupitia fursa zilizopo.
Tanzania na India zimekuwa na ushirikiano mzuri na wakudumu wa kidipolomasia na kiuchumi ambao umeendelea kuzinufaisha nchi zote mbili. Mfano, Juni 2015 Tanzania ilinufaika na mkopo kutoka nchini India wa upanuzi wa mradi wa maji kutoka Ziwa Vikitoria kwenda Mkoani Tabora, mradi huu ambao unanufaisha zaidi ya watu 1,433,004 ulikamilika mwaka 2019.
India ilianzisha Ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 1961 (wakati huo ilijulikana kama Tanganyika), hii ilikuwa kabla Tanganyika haijapata uhuru, na Tanganyika ilianzisha Ubalozi wake nchini India mwaka 1962, mara baada ya kupata Uhuru.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Brigedia Generali Wilbert Ibuge, akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini India Balozi Baraka Luvanda, Balozi huyo alipowasili Wizarani kufanya mangumzo na Katibu Mkuu mjini Dodoma, leo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇