LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 8, 2021

UAMUZI WA ICC: USHINDI KWA WAPALESTINA

 

  • Uamuzi wa ICC; ushindi kwa Wapalestina

Kufuatia ombi la Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa ajili ya kuchunguza jinai za utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya taifa la Palestina, majaji wa mahakama hiyo wametoa uamuzi wakisema kuwa mahakama hiyo inafaa kisheria kuchunguza jinai za kivita katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Hukumu hiyo imetolewa katika hali ambayo mwezi Disemba 2019, Fatou Bensouda, mwendesha mashtaka mkuu wa ICC alisema kuwa kulikuwepo na ushahidi wa kutosha uliothibitisha kwamba kuna jinai za kivita ambazo zilitekelezwa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yakiwemo maeneo ya Quds Mashariki na vile vile katika Ukanda wa Gaza. Kufuatia kutolewa tuhuma za jinai za kivita dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, ombi lilitolewa kwa majaji wa Mahakama ya ICC kwanza wachunguze iwapo mahakama hiyo ilifaa kisheria kufanya uchunguzi kuhusu jinai hizo au la.

Hivi sasa mahakama hiyo imetia uamuzi ikithibitisha kuwa inayo ustakihi wa kisheria wa kuchunguza na kufuatilia jinai zilizotekelezwa na utawala haramu wa Israel katika ardhi unazozikalia kwa mabavu tokea mwaka 1967, yaani Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, unaojumuisha pia Quds Mashariki. Kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mipaka ya 1967 inahesabika kuwa mipaka ya ardhi za Palestina na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi hizo ni kinyume cha sheria, jambo ambalo limekuwa likikukwa wazi na utawala wa Kizayuni.

Fatou Bensouda

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilibuniwa mwaka 2002 kwa ajili ya kuchunguza na kufuatilia jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu, mauaji ya kimbari na jinai nyinginezo kama vile ubakaji katika maeneo ya vita, lakini Israel haijajiunga na mahakama hiyo na wala haiitambui rasmi. Hukumu ya hivi karibuni ya ICC imeukasirisha sana utawala wa kibaguzi wa Israel ambapo Benjamini Netanyahu, waziri mkuu wa utawala huo ameituhumu mahakama hiyo yenye itibari ya kimataifa akidai kuwa hukumu hiyo imethibitisha kwa mara nyingine kwamba hiyo ni taasisi ya kisiasa na wala si ya kisheria.

Hasira hiyo ya watawala wa Israel inaeleweka kwa kutilia maanani kwamba hatua ya ICC ya kuchunguza jinai za kivita katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, itafichua na kuanika wazi jinai zilizotendwa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina na hata huenda ikapalekea viongozi wengi wa utawala huo kufuatiliwa kisheria na hatimaye kukamatwa na kufikishwa kizimbani kutokana na jinai hizo.

Ahmad Abulghait, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) amesema: Suala la Palestina limesahaulika sana na kuna mtazamo usiokuwa wa usawa kuhusu suala hili; yaani suala la mzozo wa Palestina na Israel linatazamwa kwa mtazamo mmoja tu tena kwa maslahi ya utawala wa Israel. Ni kana kwamba upande mwingine ambao ardhi zake zinakaliwa kwa mabavu haupo kabisa au kwamba Wapalestina wametakiwa wakubali na kuishi chini ya mazingira ya kutwishwa bila kuteta wala kulalamika.

Ahmad Abulghait

Ujenzi wa vitongoji visivyo vya kisheria, Wapalestina kutekwa nyara katika kambi za utawala haramu wa Israel, kuuawa kigaidi na kinyama wakiwa mitaani na kushambuliwa kwa mabomu bila huruma ni baadhi ya jinai zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wa Palestina wasio na mtu wa kuwatetea. Jinai hizo zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni kutokana na huduma kubwa iliyotolewa kwa utawala huo ghasibu na utawala wa Donald Trump, rais wa Marekani aliyeondoka madarakani karibuni. Jinai hizo zote zinahesabiwa kuwa ni jinai za kivita. Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa hivi karibuni na majaji wa mahakama ya ICC, sasa mahakama hiyo itakuwa na haki ya kufuatilia jinai zote za kivita zilizotekelezwa na utawala huo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Gaza na vilevile eneo la Quds Mashariki.

ICC hatimaye imeamua kuingilia kati na kuchunguza jinai za kutisha zilizofanywa na utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya watu wa Palestina, taifa ambalo limeteseka kwa miaka mingi chini ya ugaidi na ukatili wa kinyama wa Wazayuni wasio na huruma. Kwa msingi huo hatua hiyo ya ICC ni suala muhimu na ushindi mkubwa kwa taifa la Palestina. Pamoja na hayo kuna wasi wasi mkubwa kwamba huenda Marekani na washirika wa Ulaya wa Israel wakashirikiana kwa karibu na kutumia kila mbinu kwa ajili ya kutoa mashinikizo ya kuizuia mahakama ya ICC itekeleze vizuri shughuli zake za kuchunguza jinai hizo za utawala wa Israel na hivyo kutofikiwa natija inayotarajiwa na Wapalestina.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages