Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza.
Dodoma, Tanzania
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewaagiza Wenyeviti wa Mabaraza ya ardhi na Nyumba ya wilaya kutumia lugha ya Kiswahili katika kuandika hukumu.
Lukuvi alitoa maagizo hayo tarehe 5 Februari 2021 jijini Dodoma alipozungumza na Wenyeviti pamoja na Wasajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwa nchi nzima kupitia Video (Video conference).
‘’Nasisitiza wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mtumie lugha ya Kiswahili wakati wa kuandika hukumu zenu kama alivyoagiza mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli na nitashangaa kumuona mwenyekiti akiandika hukumu kwa lugha ya kiswahili’’ alisema Lukuvi
Aidha, Lukuvi aliwataka pia wenyeviti hao wa Mabaraza kuchapa hukumu za maamuzi wanayotoa wao wenyewe bila kutegemea Makarani na hukumu hizo zitoke kwa wakati na kusisitiza kuwa katika dunia ya leo suala la uzembe halina nafasi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema kuwa, pamoja na kuwepo uchache wa watumishi kwenye baadhi ya ofisi za Mabaraza ya Ardhi lakini watendaji hao wanatakiwa kuwajibika na kuacha visingizio pamoja na kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa serikali iko katika juhudi za kuhakikisha inajaza nafasi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, hivi sasa ni wajibu wa watendaji wa mabaraza ya ardhi kufanya kilicho sahihi na kuwa wabunifu sambamba na kuwajibika kwa kutoa hukumu kwa wakati na kusisitiza wananchi masikini wanategemea sana matumizi ya Kiswahili.
‘’Maamuzi yetu kama wenyeviti wa Mabaraza yawe rahisi na sisi tuwe wa kwanza kuwasaidia wananchi na kila mwenyekiti atekeleze maamuzi haya kwa lugha ya Kiswahili’’ alisema Lukuvi
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, wapo wananchi waliokosa haki zao ama kuchelewa kukata rufaa kutokana na kutokujua kilichoandikwa katika hukumu kwa kuwa kimeandikwa kwa kiingereza.
Kwa upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Stella Tullo aliwataka Wenyeviti wa Mabaraza kuanza kutekeleza maagizo ya Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mapema kwa kuzingatia sheria na taratibu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇