Muonekano wa Taa za kuongozea magari zilizosimikwa na Kikosi cha Umeme (TEMESA) katika eneo la Simu 2000 jijini Dar es Salaam.
Picha ni nguzo za Taa za barabarani ambazo zinatengenezwa na mafundi kutoka Kikosi cha Umeme (TEMESA) katika karakana yake iliyopo Keko jijini Dar es Salaam.
Mafundi kutoka Kikosi cha Umeme (TEMESA) wakiendelea na kazi ya kusimika umeme katika Taa za barabarani zilizofungwa katika makutano ya Sam-Nujoma na Simu 2000 jijini Dar es Salaam.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA)
************************
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kupitia Kikosi Cha Umeme ambacho kinasimamia kazi za kandarasi za mifumo ya Umeme, Elektroniki, TEHAMA, Viyoyozi pamoja na Usimikaji na matengenezo ya taa za barabarani umeanza kazi ya kusimika taa za kuongozea vyombo vya moto (traffic lights) katika barabara za Shekilango, Sam-Nujoma na Ubungo Interchange jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mwandishi wetu mapema leo, Meneja wa Kikosi cha Umeme anayesimamia mradi huo Mhandisi Pongeza Semakuwa amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika haraka iwezekanavyo ili uanze kutumika na taa hizo zinasimikwa kwa kutumia fedha za ndani zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
‘‘Katika barabara ya Shekilango, taa hizo zinasimikwa katika makutano yapatayo matano kwa gharama ya shilingi milioni 700, Katika barabara ya Sam-Nujoma taa hizo zina simikwa katika makutano matatu yaliyopo Mawasiliano tower na Simu 2000 kwa gharama ya shilingi milioni 350, wakati katika makutano ya Ubungo ‘flyover interchange’ kazi hii imefanyika kwa kushirikiana na mkandarasi wa mradi wa daraja hilo kwa gharama ya shilingi milioni 70,’’ alisema Mhandisi Pongeza.
Mhandisi Pongeza pia ameongeza kuwa kazi hizo zinafanyika kwa haraka na kwa muda mfupi wa takribani miezi mitatu kwa kuzingatia kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano, amesisitiza kuwa gharama za mradi huo zimekuwa nafuu tofauti na hapo awali kwasababu nguzo zote zinazotumika kama malighafi za kutengenezea taa hizo zinatengenezwa katika karakana ya Kikosi hicho zilizopo Keko Darajani jijini Dar es Salaam.
Hapo awali nguzo hizo pamoja na malighafi zake zilikuwa zikinunuliwa wa gharama kubwa kutoka nje ya nchi na hivyo kusababisha miradi hiyo kuwa ya gharama kubwa na wakati mwingine kuchelewa kumalizika kwa wakati kutokana na kuchelewa kufika kwa malighafi zilizokuwa zikitumika Kutoka nje ya nchi zilipokuwa zinaagizwa.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika hivi karibuni na kuanza kufanya kazi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇