*******************************************
NA SULEIMAN MSUYA
RAI imetolewa kwa Waislam na Watanzania kwa ujumla kumuomba Mwenyezi Mungu, kutoa sadaka na kuchukua tahadhari ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya COVID-19 (Corona).
Rai hiyo imetolewa na Sheikh Hashim Rusaganya wakati akitoa hotuba ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Mtambani wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Sheikh Rusaganya anaungana na Rais John Magufuli ambaye amekuwa akisisitiza kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuchukia tahadhari katika mapambano dhidi ya corona kwa kuwa ndiye muweza wa yote.
Akitoa hotuba hiyo Rusaganya amesema ni wazi kuwa wanasayansi na wataalam wote wa tiba duniani wameshindwa kupata dawa ya kutibu corona hivyo njia sahihi ya kupambana na janga hilo ni kumuelekea kwa Mwenyezi Mungu.
Amesema dunia inapaswa kutambua Mwenyezi Mungu pekee ndiye mponyaji na mletaji wa magonjwa hivyo ni wao kuchagua kuelekeza nguvu zao kwake kwa kuomba dua, kufanya ibada, kutoa sadaka na kuchukua tahadhari.
Amesema Tanzania ni sehemu ya dunia hivyo maambukizi hayo yanaweza kuwepo na kuleta madhara.
“Naomba nitumie nafasi hii kuwaamba ndugu zangu waislam na Watanzania kwa ujumla tiba ya corona ni kumuelekea Mwenyezi Mungu na kumlilia, lakini pia tutoe sadaka kwani wengi wamepona kwa kutoa sadaka.
Katika Sura ya 50, Aya ya 51 kwenye Qur’an inaelekeza kuwa kutoa sadaka ni njia sahihi ya kutoandolea magonjwa na hata katika hadithi nyingi za Mtume Mohammed S.A.W ameeleza hivyo hivyo naamini tukijikita huko tutaweza kunusurika.
Mimi namuunga mkono Rais Magufuli kwani amekuwa akisisitiza tumuelekee Mungu lakini pia tuchape kazi ugonjwa huu hauna dawa ya moja kwa moja,” amesisitiza.
Amesema Rais ni baba wa nchi anavyowataka mchukue tahadhari na kufanya kazi anataka nchi iendelee kuwa imara kwa kila sekta.
Sheikh Rusaganya amesema jamii imemsahau Mungu katika mambo mazito hivyo inapaswa kubadilika ili kuwa salama.
Amesema iwapo kila mmoja atamuelekea Mungu na kuchukua tahadhari Tanzania itakuwa salama.
“Mwenyezi Mungu ndiye analeta maradhi na ndiye atatuponya kinachotakiwa ni sisi kusimama kwenye misingi ya dini na hili Rais Magufuli anasisitiza kila kukicha,” ameongeza.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇